ILI kuchukua
fomu ya kugombea urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) unatakiwa kuwa na
shilingi 500,000 na uchaguzi utafanyika mkoani Dodoma Agosti 12 mwaka huu.
Hayo
yamesemwa leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, msomi Wakili
Revocatus Kuuli alipoongea na wandishi wa habari kusoma tangazo la uchaguzi na
nafasi zinazogombewa.
“Anayegombea
nafasi ya rais fomu itakuwa shilingi 500,000,
makamu wa rais sh. 300,000 na wajumbe wa kamati ya utendaji sh 200,000,”
alisema Wakili Kuuli.
Pia Wakili
Kuuli alisema sifa za mgombea wa nafasi ya urais na makamu wa rais anatakiwa
kuwa na kiwango cha elimu isiyopungua shahada moja, mwenye utu na uwezo wa
kuiwakilisha TFF ndani na nje ya nchi.
Aidha sifa
zingine za jumla anatakiwa kuwa mtanzania, elimu ya kidato cha nne, uzoefu
katika uendeshaji wa soka kwa miaka mitano, awe na umri angalau miaka 25.
Asiwe na
hatia yoyote ya kosa la jinai au kifungo kisicho na mbadala wa faini, awe
amewahi kuwa mchezaji wa soka, kocha, refa
au kushiriki katika uendeshaji wa mpira wa miguu katika ngazi ya mkoa au
daraja la kwanza.
Wakili Kuuli
alisema nafasi zinazogombewa ni rais, makamu wa rais na wajumbe 13 wanaowakilisha
kanda 13 na mchakato wa uchaguzi utabandikwa kwenye mbao za matangazo kuanzia
kesho.
“Fomu za
kuomba uongozi zitaanza kutolewa Juni 16 na mwisho wa kurudisha ni Juni 20 na
zitakuwa zinapatikana kwenye Ofisi za TFF, Ilala na katika tovuti ambayo ni www.tff.or.tz,”
alisema Wakili Kuuli.
Wakili Kuuli
alisema Juni 21-23 kutafanyika kikao cha mchujo wa awali wa wagombea na
kuwaandikia barua za kuwajulisha juu mchujo wa awali kabla ya Juni 24-25
kuchapisha na kubandika orodha ya awali ya wagombea.
Kipindi cha
kuweka pingamizi ni Juni 26-28 na pingamizi zinatakiwa kuwekwa na wagombea
pekee na Juni 29 hadi Julai Mosi kupitia
pingamizi zote kufanya usaili wa wagombea.
Alisema
kamati ya uchaguzi itatangaza matokeo ya awali ya usaili Julai 2-3 na
sekretarieti itawasilisha masuala ya kimaadili kwenye kamati ya maadili Julai 4-6.
Wagombea
watakuwa na fursa ya kukata rufaa kwa maamuzi ya masuala ya kimaadili kwenye
kamati ya rufaa ya maadili ya TFF baada ya kamati ya maadaili kutangaza matokeo
ya maamuzi ya kamati hiyo Julai 15-17.
Kipindi cha
kusikilizwa na kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF, Julai 29 hadi Agosti 4 na
orodha ya mwisho ya wagombea na kutangazwa Agosti 5-8 na kampeni kwa wagombea
wote itaanza Agosti 7-11.
Wakili Kuuli
alisema watashirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (TAKUKURU)
kuzuia na kudhibiti vitendo vya rushwa kwa wagombea na ikithibitika mgombea
ametoa rushwa watamfikisha katika vyombo vya sheria.
No comments:
Post a Comment