WANAWEZA
kuwa wamemaliza Ligi Kuu ya England (EPL) katika nafasi mbovu ukilinganisha na
mabingwa wapya wa Hispania, Real Madrid, lakini Manchester United ndio klabu
tajiri zaidi duniani.
Baada ya kuweweseka
tangu kuondoka kwa kocha wao mkongwe, Alex Ferguson na kuwajaribu David Moyes
na Louis van Gaal bila mafanikio ya kuridhisha kwenye soka na nje ya dimba,
sasa United wanakuja.
Wamemaliza
msimu wa 2016/17 chini ya kocha maarufu na mwenye makeke, Jose Mourinho wakiwa
nje ya timu nne bora England, lakini wakafanikiwa kuingia kwenye Ligi ya
Mabingwa Ulaya (UCL) watakakokwenda kupigana vikumbo na akina Real, Barcelona,
Bayern Munich, Juventus na vigogo wengine wa Ulaya. Walifika huko kupitia
uchochoro wa Ligi ya Europa.
Na sasa
habari njema inakuja kwa jamaa wa Old Trafford, kwamba heshima imerudi mjini,
kwa sababu sasa ndio klabu wanaoongoza duniani kwa utajiri, ambapo wamekutwa
kuwa na utajiri wa pauni pauni bilioni 2.7, katika thamani ya kibiashara.
Taarifa
iliyotolewa na kampuni ya kitaaluma ya KPMG inasema kwamba hali hiyo hupimwa
kwa kutazama ingegharimu kiasi gani cha fedha kuinunua klabu ya soka, ikielezwa
kwamba haki za utangazaji ni moja ya vigezo vilivyowanyanyua United.
Man U
wamefanikiwa kuwapiku matajiri wa Hispania na wazuri kisoka, Real Madrid na
Barcelona licha ya kwamba klabu hii inayomilikiwa na familia ya Glazer ina deni
kubwa la pauni karibu nusu bilioni.
Man U
wanafuatiwa, kwa utajiri wa kibiashara, na Real Madrid, Barcelona, Bayern Munich,
Arsenal, Chelsea, Liverpool, Juventus, Tottenham Hotspur, Borussia Dortmund,
Atlético Madrid, Schalke, Milan, Leicester, Everton, Roma, Inter, Napoli,
Galatasaray, Fenerbahce, Benfica na Lyon.
Tafsiri yake
ni kwamba akitokea mtu au kampuni au shirika wanaotaka kununua klabu ghali
zaidi duniani itakuwa ni Manchester United.
No comments:
Post a Comment