Kitabu hiki
nimekigawanya kwa kuzingatia umri wa wachezaji hivyo basi kitabu hiki kimefanya
vipatikane vitabu vingine vitatu ambavyo vinabeba jina hilo la boresha na
endeleza kipaji chako cha soka.
Kitabu cha kwanza ni
cha wachezaji kuanzia umri wa miaka 6-14, kitabu cha pili ni cha wachezaji
kuanzia umri wa miaka 14-17, kitabu cha tatu ni cha wachezaji kuanzia umri wa
miaka 17 -20 huku kitabu chenyewe ambacho ndio kikubwa kitakuwa kwa wachezaji
kuanzia umri wa miaka 6-20,” anasema Juma Kimaya ambaye ni mwandishi wa vitabu
hivyo.
Juma ni nani?
Juma ni kijana wa
kitanzania mwenye umri wa miaka 20, alizaliwa na kupata elimu ya msingi wilaya
ya Nzega, Tabora lakini baadae alihamia Dar es Salaam. Alipata elimu ya
sekondari kwenye shule ya sekondari ya Kibasila iliyopo Dar es Salaam na
alihitimu kidato cha nne mwaka 2014.
Alipokuwa na umri wa
miaka mitano alianza kucheza soka katika timu za mitaani Tabora kabla ya
kuhamia Dar es Salaam na kuendelea kucheza huku akiwa anasoma.
Mwaka 2010 akiwa
kidato cha kwanza aliichezea Yanga B yenye maskani yake mitaa ya Jangwani na
Twiga Dar es Salaam lakini anakiri
hakucheza kwa mafanikio ndio akapata wazo la kuandika kitabu kikiwa mwongozo
wake katika kujifunza mchezo wa soka.
Baada ya kupata wazo
hilo alimweleza kocha wake wa Yanga B, Anthony Chibasa ambaye alimshauri amuone
aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Sunday
Kayuni ambapo alionana naye na kumpatia alichokihitaji.
Baada ya kuhitimu
kidato cha nne mwaka 2014 wakati akicheza soka aliumia goti na huo ndio ukawa
mwisho wa kuacha kusakata kabumbu na kwenda Mwanza kuuguza goti.
Safari ya kuandika kitabu inaanza
Anasema wakati
akicheza soka aliandika muswada wa kumwongoza katika uandishi wa kitabu chake,
lakini pia ulimsaidia kwenye kuboresha kiwango cha uchezaji japo ndoto ya kuwa
mchezaji mahiri ilizimika baada ya kuumia goti.
Baada ya kuachana na
soka akaanza kuuweka muswada wake usomeke na kueleweka kwa wachezaji wenzake
kwani alitambua wachezaji wengi wa Tanzania hutumia vipaji pekee na kukosa
elimu ya mchezo wa soka huku akitambua soka huleta uzalendo, hujenga afya na
hutoa ajira kwa vijana.
Ili kufanikisha ndoto
ya kuandika kitabu chake kwa ufasaha alilazimika kusoma kozi ya awali ya ukocha
iliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambayo iliendeshwa na Mkufunzi
Michael Bundala.
Kimaya anasema kozi
hiyo ilimsaidia kuboresha uandishi wa kitabu chake baada ya kumalizika alimpa Kayuni maswada ili amwandikie Dibaji.
Katika kuboresha
muswada anasema alilazimika kuwatafuta wataalamu wa mchezo wa soka ili wapitie
muswada wake kabla ya kuchapisha kitabu baada ya kuongea na Kayuni.
Miongoni mwa
wataalamu aliowaona ni Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF wa sasa, Salum Madadi na
aliyekuwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga
ndio walimshauri kukigawa kitabu kwa kuzingatia umri.
Pia alipata maoni ya
kocha Bundala na Mkufunzi Dk Jonas
Tiboroha wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao kila mmoja alimwandikia ujumbe
ambao unapatikana kwenye kitabu. Mwisho alikwenda serikalini kupitia Baraza la
Michezo la Taifa (BMT)ambapo walimpongeza kwa kazi yake na Katibu Mkuu Mohamed
Kiganja alimwandikia ujumbe.
“Hawa wote kwa namna
moja au nyingine walichangia kitabu hiki kiwe bora kwa mchezaji,” anasema
Kamaya.
Yaliyomo kwenye kitabu
Kitabu kimesheheni
mawazo mbalimbali ya wadau wa soka hivyo kitaongeza kasi ya kukua kwa soka la
Tanzania.
Kwa kifupi kitabu
kina sura zifuatazo ambazo zitamsaidia mchezaji kuwa bora kiuchezaji sasa na
baadae.
Sura mojawapo ni
maana ya mchezo wa mpira wa miguu na mambo yote muhimu ambayo ni lazima mchezaji
awe nayo kabla ya kuingia uwanjani.
Sura hii imeeleza
vitu muhimu ambavyo vi vema mchezaji akaviweka sawa kabla hajaingia uwanjaini
kama akili timamu na nidhamu, afya ya mwili, umbile, lishe bora na usafi wa
mavazi na mwili bila kusahau kupumzika.
Pia kuna sura
inayoeleza mazoezi ya mwili na mpira, sura hii mchezaji atajifunza mazoezi ya
mwili ambayo yatamfanya kuwa na utimamu
wa mwili, hapa mchezaji atajifunza mazoezi ya pumzi, mazoezi ya ukakamavu,
mazoezi ya wepesi wa mwili, mazoezi ya kukimbia kwa kasi na mazoezi ya viungo
vya mwili.
Mazoezi ya mpira
mchezaji atajifunza kutumia miguu yake
kwani ni muhimu ili aweze kukabili tukio la kimchezo na mguu husika kwa
wakati muafaka, atajifunza namna ya kufunga mabao kwenye magoli madogo na
makubwa na kucheza mazoezi kwenye eneo dogo na uwanja mzima.
Sura nyingine
mchezaji atajifunza mazoezi ya mwili na mpira wa miguu kwa pamoja, sehemu za
mpira wa miguu, sheria za mpira wa miguu na majukumu yake ndani ya uwanja.
Pia kuna sura
inayoitwa utulivu katika mchezo wa soka ambayo hupatikana kwenye nguzo nne
ambazo ni utazamaji, kujiamini, umakini na ukimbiaji na sura nyingine ni
historia fupi ya mpira wa miguu duniani.
Kwenye kitabu hiki
mchezaji atakutana na maelezo yaliyojitosheleza na michoro inayovutia yenye
kumpa mifano inayofanyika kwa vitendo na mwisho kuna vifupi vya maneno ambayo
itamsaidia mchezaji kutambua maana ya maneno yaliyotumika ndani ya kitabu.
Ushauri wa mwandishi kwa wasomaji
Anasema siyo
wachezaji tu wanaweza kukitumia kitabu chake bali pia walimu wa soka wanaweza kukitumia kwa kuwapatia mafunzo
wachezaji wachanga kulingana na umri kwani wana uelewa tofauti katika kupokea
mafunzo. Ili mchezaji aweze kufikia kiwango bora ni vizuri akapitia katika
malezi yafuatayo kwasababu inachukua muda si chini ya miaka 10 na saa 10,000
kwa mchezaji chipukizi kuwa mkomavu.
Anasema wazazi wana
mchango mkubwa wa kuwafanya watoto kuwa wachezaji wazuri kwa kuwajumuisha
kushiriki mazoezi ya mpira wakiwa na umri mdogo.
Uwepo wa vyuo vya
michezo utasaidia kuibua vipaji vya wachezaji na kuviendeleza kwa kuwapatia
mafunzo ya mpira wa miguu na elimu.
Pia taasisi za
michezo zenye dhamana zinahusika kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya mpira wa
miguu kwa kuanzisha mipango ya maendeleo ya wachezaji wakiwa na umri mdogo.
“Michezo ikisimamiwa
na kuendeshwa vizuri katika shule husaidia kuibua vipaji vyenye uelewa mzuri wa
mpira wa miguu na elimu kwani kipaji hakijitokezi tu bali hugunduliwa na ni
njia ndefu kufikiwa,” anasema.
Mwandishi huyo
anamaliza kwa kunukuu maandiko ya Dk Tiboroha: “Wazee wetu wa zamani walikuwa
sahihi kusema kwamba busara ya mtu haipimwi kwa umri au elimu”.
Pia ananukuu ya
Katibu Mkuu wa BMT: “Tanzania yetu tutaijenga wenyewe”. Nukuu hizi ni
zinapatika kwenye kitabu hiki ambacho kimechukua miaka kumi kukamilika.
Wito
Anatoa wito kwa wadau
kuungana naye ili elimu iwafikie wachezaji wote waliopo ndani ya nchi na nje. “Naomba
wadau wanisaidie kuchapisha kitabu hiki ili kiweze kusambazwa kwani lengo langu
ni kuwafikia wachezaji na watu wote wanaopenda soka ila sina fedha”.
Anasema kwa
anayehitaji kushirikiana naye anapatikana kwenye namba 0717100042 au barua pepe
jumakimaya3@gmail.com
Shukrani
Kimaya anawashukuru
wadau mbalimbali waliofanikisha kuandika kitabu chake kwa namna yoyote. Kipekee
anaishukuru BMT, TFF, Kayuni, Katibu Mkuu wa Chama cha Makocha (TAFCA) Bundala,
Mkufunzi wa elimu ya viungo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Tiboroha na
Kanali mstaafu na mmiliki wa shule ya michezo Lord Barden, Idd Kipingu.
Pia wazazi wake Eva
Kachala na Mohamed Rashid kwa malezi bora na elimu waliyompatia na hatimaye
kuweza kuandika kitabu ambacho leo kitasaidia kukuza soka la Tanzania.
No comments:
Post a Comment