TAIFA Stars
imeaga rasmi katika mbio za kuwania kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika
(Afcon), itakayofanyika mwakani nchini Gabon.
Safari ya
Stars imehitimishwa leo, baada ya kufungwa mabao 2-0 na Misri kwenye mchezo
uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, ukiwa ni mchezo wa kundi G.
Matokeo hayo
yanawafanya Misri wamalize mechi za Kundi G wakiwa na pointi 10 baada ya mechi
nne, wakishinda tatu na kutoka sare moja, wakati Tanzania inabaki na pointi
yake moja na inashika mkia nyuma ya Nigeria yenye pointi mbili.
Stars
ilikuwa na kibarua kigumu, kwani ilikuwa inatakiwa kushinda mabao zaidi ya 3-0
dhidi ya Mafarao hao ili iweze kufuzu kwa michuano hiyo kwa mara ya kwanza
tangu mwaka 1980.
Katika
mchezo wa kwanza dhidi ya Misri uliopigwa jijini Alexandria, Stars ilifungwa
mabao 3-0 na baada ya kujitoa kwa Chad katika kundi hilo la G, Stars ilikuwa na
karata moja ya kutakiwa kuifunga Misri ili iweze kufufua matumaini ya kufuzu
kwa michuano hiyo.
Misri
walianza kuhesabu bao la kwanza katika dakika ya 43 lililofungwa na Mohamed
Salah, baada ya kupiga mpira wa faulo iliyosababishwa na Haji Mwinyi na shuti
lake lilikwenda moja kwa moja wavuni.
Kipindi cha
pili kilianza kwa Misri kufanya mabadiliko kwa kumtoa Mohamed Ibrahim na
kumuingiza Amr Mohsen.
Nahodha wa
Stars, Mbwana Samatta anayecheza soka la kulipwa nchini Ubelgiji katika Klabu
ya Genk, alikosa penalti katika dakika ya 53 baada ya Himid Mao kuchezewa rafu
ndani ya eneo la hatari na Mohsen.
Misri
ilipata bao lake la pili katika dakika ya 58, mfungaji akiwa ni yule yule,
Salah ambaye anaichezea Klabu ya AS Roma ya Italia, baada ya kumzidi mbio beki
Aggrey Moris.
Stars, licha
ya kufanya mabadiliko katika dakika ya 61 kwa kumuingiza John Bocco ambaye
alichukua nafasi ya Elias Maguli, lakini hadi kipenga cha mwisho kinalia
hawakuweza kupenya ngome ya Misiri na matokeo kubakiwa kuwa 2-0.
Stars: Deo
Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk68,
Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Himid Mao, Thomas Ulimwengu/Deus Kaseke dk73,
Mwinyi Kazimoto, Elias Maguli/John Bocco dk62, Mbwana Samatta na Farid Mussa.
Misri: Essam
Kamal Tawfik, Alg Gabr Mossad, Ramy Hisham Abdel, Mohamed Abdel Sayed, Abood
Abdulrahamn Amed, Tarek Hamad Hamed, Mohamed Nasser Elsayed, Mohamem Ahmed
Ibrahim, Abdallah Mahamoud Said na Nagram Mohsin Fahmy.
No comments:
Post a Comment