JIJI
la Dar es Salaam leo lilisimama kwa muda, wakati mabingwa wa Tanzania, Yanga
walipowasili wakitokea Angola walikofuzu hatua ya makundi ya michuano ya Kombe
la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC).
Mamia
ya mashabiki wa Yanga walianza kumiminika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere,
Dar es Salaam kuanzia saa tano asubuhi na hadi kufikia saa nane mchana hali
uwanjani hapo ilikuwa si ya kawaida.
Pia
mashabiki wa Yanga walijipanga barabarani katika maeneo mbalimbali kuanzia
Uwanja wa Ndege, Kipawa, Vingunguti na Tazara, ambapo mara kadhaa msafara wa basi la wachezaji wa Yanga uliokuwa
ukiongozwa na bodaboda kadhaa ulilazimika kusimama mara kwa mara sababu ya
mashabiki walikuwa wanataka kuwaona.
Kivutio
kikubwa katika mapokezi hayo alikuwa kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ aliyepangua
penalti ya dakika ya 90, ambaye mashabiki walikuwa wakimgombea kutaka kumbeba.
“Ahsanteni,
nimefurahishwa na mapokezi, tulienda kufanya kazi ngumu, tunawaahidi raha
zaidi,” alisema Dida na kuungwa mkono na Haruna Niyonzima kiungo mahiri wa
Yanga na kiungo mwingine, Thabani Kamusoko.
Shamrashamra zilizopambwa na mabango yenye ujumbe
mbalimbali na vijembe, sambamba na ngoma
za singeli kwa mashabiki wa Yanga, vilitawala.
Mashabiki
walionekana karibu na lango la kutokea wageni mashuhuri ‘VIP’ wakisubiri kwa
hamu kuwaona wachezaji ambapo saa 8.50 ndege yao ilitua ikitokea Afrika Kusini
na baada ya taratibu walitoka nje ya uwanja na shangwe za: 'Dida..Dida.. Dida’
zilisikika.
Mashabiki
walikuwa wenye uso wa furaha wakizingira wachezaji waliokuwa wakielekea kwenye
gari lao, na bado utitiri ulisindikiza msafara huo na kusalimiana na mashabiki,
ambao walikuwa wakitembea kwa miguu na wengine kwenye magari hadi kwenye Ofisi
za Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam eneo la
Banda la Ngozi.
Akizungumza
na waandishi wa habari baada ya kutua, Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi
alisema ushindi huo wametoa zawadi kwa Watanzania wote.
Alisema
wanashukuru sehemu ya mafanikio hayo yametokana na Mwenyekiti Manji ambaye amekuwa akishirikiana nao katika kuhakikisha
timu inafanya vizuri.
Naye
nahodha wa Yanga, Nadir Haroub alisema mechi ilikuwa ngumu kwani hata waamuzi
walionekana kuibeba timu pinzani, lakini wao walijua kilichowapeleka na
kupigana kwa ajili ya kufanya vizuri.
Alisema
fujo zilizotokea kule hakuwahi kuziona katika maisha yake ya soka, na kwamba
kwa vile wao walikuwa wanataka ushindi walicheza mpira na kutimiza lengo
walilokusudia.
Timu
hiyo ilitarajiwa kuondoka jana jioni kwa ndege ya kukodi kuelekea Songea ambako
Jumapili itacheza na Majimaji katika kumaliza Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga
Jumatano ilifuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kutokana na matokeo ya mchezo wa uliofanyika mjini
Dundo, Angola dhidi ya Sagrada Esperanca ya huko, ambapo Yanga ilifungwa bao
1-0.
Kutokana na matokeo hayo, Yanga imefuzu kwa
jumla ya mabao 2-1 baada ya mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam, Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Katika
mchezo wa Dar es Salaam lilikuwa bao zuri la Simon Msuva aliyefunga kwa kichwa
kufuatia majalo ya chini chini ya Geoffrey Mwashiuya, akawaamsha vitini
mashabiki wa vijana hao wa Jangwani. Bao jingine lilifungwa na chipukizi Matheo
Anthony kwa mkwaju mkali.
Kwa
kuingia hatua ya makundi, Yanga imeandika historia mpya katika soka nchini kwa
kuwa klabu ya kwanza Tanzania kufuzu hatua hiyo katika mashindano hayo, lakini
ni mara ya pili kufuzu hatua ya makundi kwa mashindano makubwa Afrika baada ya
kufanya hivyo mwaka 1998 katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba
ya Dar es Salaam nayo ilifuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka
2003 kwa kuitoa Zamalek ya Misri.
Yanga
iliangukia Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC), baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri hatua
ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ililazimishwa sare
ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa mabao 2-1 Alexandria, Misri.
Ilizitoa
Cercle de Joachim ya Mauritius kwa mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0
nyumbani kabla ya kuitoa APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1
Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
Yanga
sasa inaungana na miamba mingine saba Afrika na inasubiri droo ya upangaji wa
makundi wiki ijayo ili ijue itakuwa kundi gani.
Timu
nyingine zilizofuzu hatua ya makundi na nchi zao katika mabano ni MO Bejaoa
(Algeria), Al Ahli Tripoli (Libya), FUS Rabat (Morocco), Kawkab (Morocco), ES
Sahel (Tunisia), Medeama (Ghana) na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo (DRC).
Wachezaji
hao walizungumza na Mwenyekiti Manji kwa dakika kadhaa, ambapo waandishi
hawakuruhusiwa kuingia na baada ya kikao hicho Mkuu wa Idara ya Habari na
Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro alisema kila mchezaji ameahidiwa gari.
“Wachezaji
wamezungumza na Mwenyekiti na amewaahidi kuwapa kila mmoja gari kwa hatua hii
waliyofikia. Sasa ni gari gani hiyo itakuwa siku nyingine.
“Lakini
nataka kuwahakikishia kwamba mtawaona wachezaji wanabadilisha maisha yao muda
si mrefu. Ila ninachotaka kuwaambia sasa ni kwamba kila mchezaji ameahidiwa
kupewa gari kwa kutinga hatua hii ya makundi na amewataka wasibweteke.
“Pia
amewataka wasibweteke kwa kutinga makundi, bali wapambane zaidi na hata msimu
ujao wacheze makundi Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Muro.
No comments:
Post a Comment