NI Yanga ya kimataifa na mataji. Pengine ndivyo
unavyoweza kuzungumzia matokeo ya mchezo wa fainali ya Kombe la FA kati ya
Yanga na Azam uliochezwa leo Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na Yanga kuibuka
na ushindi wa mabao 3-1.
Kulingana na kanuni za mashindano hayo, bingwa wa Kombe
la FA huwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika
(CAF CC) msimu ujao, hivyo kwa ushindi wa jana Yanga ingepata fursa ya
kuwakilisha nchi katika michuano hiyo.
Hata hivyo, kwa vile Yanga tayari imetwaa ubingwa wa Ligi
Kuu Tanzania Bara itawakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika
ambayo ni mikubwa kwa ngazi ya klabu na kanuni kuipa Azam nafasi ya kucheza
Kombe la CAF CC.
Yanga ilipata bao la kwanza dakika ya tisa, mfungaji akiwa
Amis Tambwe kwa kichwa akiunganisha krosi ya Juma Abdul, bao lililofuatiwa na
mashambulizi makali kila upande.
Makipa Deogratius Munishi ‘Dida’ wa Yanga na Aishi Manula
wa Azam, ambao pia ni makipa wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’
kwa nyakati tofauti jana walionesha uwezo mkubwa wa kupangua michomo ya
washambuliaji katika milango yao.
Dakika ya 48, Tambwe aliifungia Yanga bao la pili
kutokana na pasi ya Simon Msuva kabla ya dakika moja baadaye Didier Kavumbagu
aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya John Bocco kuifungia Azam bao.
Kuingia kwa bao hilo kulionekana kuwachanganya Yanga
ambao katika dakika ya 81 walipata bao la tatu kupitia kwa Deus Kaseke
aliyefunga bao la tatu baada ya kupokea pasi ya Msuva. Kwa ushindi huo, Yanga
imetwaa kombe hilo na kitita cha Sh milioni 50.
Mara ya mwisho Kombe la FA lilifanyika mwaka 2002 na JKT
Ruvu Stars ya Pwani ikaibuka bingwa baada ya kuifunga Baker Rangers ya Magomeni
kwenye fainali.
Wakati huohuo, kocha wa Yanga, Hans Pluijm amesema hana
hofu yoyote na timu ilizopangwa nazo Yanga katika michuano ya Kombe la
Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC) hatua ya makundi.
Juzi Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilipanga ratiba ya
michuano hiyo, ambapo Yanga ipo Kundi A pamoja na mabingwa wa zamani wa Afrika,
TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Medeama ya Ghana na MO
Bejaia ya Algeria.
Akizungumza na gazeti hili, Pluijm alisema anaijua vizuri Mazembe na
Medeama, kwa sababu amewahi kukutana nazo mara kadhaa akiwa na timu tofauti,
hivyo haoni kama zitamsumbua katika mipango ya kucheza nusu fainali ya michuano
hiyo.
“Timu ambayo inaweza kutusumbua kwa sababu siifahamu
vizuri ni Bejaia ya Algeria, lakini baada ya ratiba kutoka tumeanza mikakati ya
kuimarisha kikosi changu,” alisema Pluijm.
Alisema Yanga ni moja ya timu kubwa na ndiyo maana
imekuwa katika nane bora Afrika, hivyo haoni sababu ya kuwa na presha kwani
wana uwezo mkubwa wa kufanya vizuri kutokana na mikakati waliyo nayo.
Katika michuano hiyo, Yanga itafungua dimba
na Mouloudia Olympique Bejaia nchini Algeria Juni 17 na itacheza na TP
Mazembe Dar es Salaam kati ya Juni 27 na 28 mwaka huu kabla ya kumaliza hatua
ya makundi pia nyumbani Julai 15 kwa kuvaa na Medeama ya Ghana.
No comments:
Post a Comment