Mpaka
sasa taarifa kutoka Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), mchezo wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kati ya Ndanda na Young Africans
umepangwa kufanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mara baada ya Yanga
kuomba hivyo na Ndanda kama timu mwenyeji kuridhia kuuhamisha kutoka
Nangwanda Sijaona wa Mtwara.
Kwa nyakati tofauti, mwishoni mwa
wiki iliyopita Young Africans ilituma maombi kwa Ndanda kadhalika TPLB
kuomba ridhaa ya mchezo huo kufanyika Dar es Salaam kwa kuwa inatarajiwa
kusafiri Jumapili alfajili kwenda Angola kwa ajili ya mchezo wa
marudiano dhidia ya Sagrada Esperanca ya Angola.
Kwa mujibu wa
taarifa kutoka TPLB, Ndanda imekubali ombi la Young Africans iliyoomba
mchezo huo uhamishwe kwa malengo ya kuisaidia Young Africans kuwahi
usafiri ndege kwenda Angola ambako wanatarajiwa kucheza na wapinzani wao
ama Mei 17 au 18, mwaka huu.
Barua ya Bodi ya Ligi kwa TFF
imesema kwamba Young Africans watatumia mchezo huo ambao Ndanda itakuwa
mwenyeji kupokea taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Ofisa
Habari wa Yanga, Jerry Muro ameishukuru Ndanda kwa uungwana wao wa
kujali maslahi ya taifa na kukubali mchezo huo kufanyika Dar es Salaam,
kabla ya Young Africans kwenda Angola.
Kanuni ya pili ya Ligi
Kuu Bara toleo la 2015/16 imeeleza wazi kuwa, “Katika mazingira maalumu,
timu inaweza kucheza mchezo wake wa nyumbani katika uwanja mwingine
endapo kuna sababu nzito na za msingi, utambulisho wa uwanja katika
mazingira haya pia unawajibika kufanywa katika kipindi cha uthibitisho
wa kushiriki ligi au kwa maombi maalumu kwa TPLB,” inasehemu kanuni
hiyo.
Kwa kuzingatia kanuni hiyo na sababu za Yanga ambazo Ndanda na
Bodi wameona kuwa ni nzito wamekubaliana kucheza mchezo huo Dar es
Salaam.
Yanga inatarajiwa kucheza na wapinzani wao, Sagrada
Esperanca ya Angola ama Mei 17 au 18, 2016. Katika mchezo wa kwanza
ulifanyika Dar es Salaam Jumamosi iliyopita Yanga iliwafunga wageni wake
mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga
inahitaji ama sare, ushindi na kama kufungwa basi si zaidi ya bao moja
ili kuindoa Esperanca katika hatua ya awali, ili kuingia hatua ya
makundi katika kusonga mbele.
No comments:
Post a Comment