TIKETI za elektroniki
zitaanza kutumika wiki ijayo katika Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya miundombinu
kukamilika.
Kauli hiyo ilisemwa na Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alipozungumza na waandishi
wa habari Dar es Salaam jana. wakati akipokea mkanda WBF kutoka kwa bondia
Francis Cheka.
“Tumekubaliana na Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) kuwa tiketi za elektroniki zianze kutumika baada ya michezo ya
Machi 8, ili TFF wamalize tiketi
walizokuwa wamechapisha,” alisema Nape.
Pia Nape alisema miundombinu
ya kuruhusu matumizi ya hizo tiketi yamekamilika kama Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa alivyoagiza alipokutana na wadau na viongozi wa vyama vya michezo hivi
karibuni.
Nape pia alimpongeza bondia
Cheka kwa kumpiga bondia wa Serbia,
Geard Ajetovic katika pambano la kuwania ubingwa WBF ambalo lilifanyika viwanja
vya Leaders Klabu, Dar es Salaam hivi karibuni.
“Kwa niaba ya Watanzania nakupongeza kwa
kumpiga Ajetovic ndani ya ardhi ya nchi yako na sisi Wizara inayosimamia
michezo tutajitahidi kuwasaidia wanamichezo wote kufanikisha malengo yao,” alisema
Nape.
Naye Cheka alitoa shukrani
zake kwa Watanzania ambao walijitokeza kumuunga mkono katika pambano hilo na
kuomba kampuni zijitokeze kuwekeza katika michezo.
No comments:
Post a Comment