Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Thursday, January 21, 2016

YANGA YAREJEA KILELENI BAADA YA KUIFUNGA MAJIMAJI 5-0





USHINDI wa mabao 5-0 iliyoupata leo dhidi ya Majimaji ya Songea umeiwezesha Yanga kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kutokana na ushindi huo wa jana katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga imefikisha pointi 39 sawa na Azam iliyochukua usukani juzi kutoka kwa Yanga, lakini uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa unairudisha Yanga kileleni.

Azam ina mabao ya kufunga 30 na imefungwa 10, wakati Yanga ina mabao ya kufunga 36 na imefungwa matano hivyo kuwa na uwiano mzuri zaidi. Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 33, ambapo timu zote zimemaliza mechi 15 za duru la kwanza.

Katika mchezo wa jana, bao la kwanza la Yanga lilifungwa dakika ya tano mfungaji akiwa Thabani Kamusoko kutokana na pasi ya Deus Kaseke.

Majimaji walitulia kutaka kusawazisha bao hilo na dakika ya 34 Marcelo Bonaventura alikosa nafasi ya kufunga baada ya shuti lake kutoka pembeni kidogo ya lango la Yanga.

Majimaji iliendelea kufanya mashambulizi ya kushtukiza, lakini umaliziaji haukuwa mzuri, hali ambayo pia iliwakuta Yanga huku washambuliaji wake Amis Tambwe na Donald Ngoma wakishindwa kutumia nafasi hizo kipindi cha kwanza.

Dakika ya 48 Yanga iliandika bao la pili mfungaji akiwa Ngoma kutokana na pasi ya Kamusoko, wakati bao la tatu lilifungwa dakika ya 56  na Tambwe.

Yanga iliendelea kulishambulia lango la Majimaji ambayo ipo nafasi ya 14 katika timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo ikiwa na pointi 12, ambapo dakika ya 76 Tambwe alifunga bao la nne kutokana na pasi ya Kaseke.

Tambwe aliifungia Yanga bao la tano dakika ya 85, likiwa la tatu katika mchezo wa jana, lakini pia likiwa la 13 tangu msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara uanze na hivyo kuongoza katika ufungaji akimuacha Hamisi Kiiza wa Simba mwenye mabao 10.

Naye Alexander Sanga anaripoti kutoka Shinyanga kuwa Mwadui jana iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mwadui, Shinyanga. Mabao ya Mwadui yalifungwa na Jerry Tegete dakika ya 22 na Fabian Gwense dakika ya 51. Bao la Kagera lilifungwa dakika ya 88 na Babu Ally.

No comments:

Post a Comment