cronaldo-e1443289001946
Staa wa Real Madrid na mshindi wa pili katika tuzo za Ballon d,or 2015, Cristiano Ronaldo (pichani) ameweka wazi kuwa kocha mpya wa timu hiyo, Zinedine Zidane anaeleweka na wachezaji wa klabu hiyo kuliko kocha aliyekuwepo awali, Rafa Benitez.
Akizungumza baada ya mchezo wa ligi kuu ya Hispania dhidi Sporting de Gijon, Ronaldo alisema tangu nafasi ya kocha kuchukuliwa na Zidane kumekuwepo na mabadiliko katika klabu hiyo hali inayochangia kupata ushindi mkubwa katika michezo yote miwili ambayo amewaongoza Zidane.
“Tunamwelewa zaidi Zidane, na hilo ndiyo soka.… nimeona mabadiliko tangu alipowasili Zidane lakini wote Zidane na Benitez wanataka vitu vizuri kwenye klabu,
“Ninajihisi vizuri zaidi nikifundishwa na Zizou na usiniulize kwanini,” alisema Ronaldo.
Aidha Ronaldo alimlinganisha Zidane na Carlo Ancelotti ambaye aliisaidia Real Madrid kushinda kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2013/2014.
“Ninaona kivuli cha Carlo ndani ya Zidane, ni mtu ambaye yupo makini na kazi yake wakati wa kufanya kazi na mcheshi mnapokuwa nje ya kazi,” alisema Ronaldo.