Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Saturday, November 14, 2015

TAIFA STARS IMEKUFA NYUMBANI






TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars leo imewatoa mashabiki wa soka vichwa chini baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya miamba ya Afrika, Algeria katika mechi ya kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2018, kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Matokeo hayo sasa yanaifanya Stars ipigane kufa kupona mjini Algiers katika mechi ya marudiano Jumatano ijayo.

Stars ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 mpaka dakika ya 70, lakini ikaruhusu Algeria kusawazisha mabao hayo ndani ya dakika nne.

Ikicheza mbele ya umati uliokusanyika kwenye uwanja huo wa Taifa, Stars ilitandaza soka safi katika kipindi chote cha kwanza huku wachezaji wake wakikosa mabao kadhaa.

Mabao ya Stars yalifungwa katika kila kipindi kupitia kwa Elias Maguli katika dakika ya 43 na Mbwana Samatta katika dakika ya 54.

Maguli alifunga bao la kuongoza baada ya kuunganisha mpira wa kurusha wa Haji Mwinyi kabla ya kuichambua ngome ya Algeria na kuujaza mpira wavuni.

Samatta, ambaye ni mfungaji bora Afrika kwa sasa, alifunga bao lake kwa shuti.

Dakika ya 65 benchi la ufundi la Stars lilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Mudathir Yahya na Maguli na nafasi zao kuchukuliwa na Said Ndemla na Mrisho Ngassa.

Mabadiliko hayo ndiyo yaliyoigharimu timu, kwani sasa ilionekana kupwaya zaidi na  Slimani Islam wa Algeria alitumia nafasi hiyo kusawazisha mabao yote mawili katika dakika ya 71 na 75 baada ya kuwazidi maarifa mabeki wa Stars.
Mbali na kasoro hizo, Stars ilianza mchezo huo kwa kasi ya kushambuliana katika dakika ya pili tu ya mchezo Farid Musa alipata nafasi nzuri ya kufunga akapaisha.

Nafasi nzuri za kufunga kama hizo pia zilipatikana kwa Samatta na Thomas Ulimwengu kwa nyakati tofauti, lakini ama walikuwa wakipaisha au mipira ilidakwa na kipa wa Algeria M’bolhi Rais.

Stars inatarajiwa kuondoka nchini kesho kuelekea Algiers kwa ajili ya mechi ya marudiano itakayochezwa Jumatano ambapo timu itakayoshinda itaingia kwenye makundi katika kinyang’anyiro hicho cha kuwania kwenda Urusi.

Stars: Ally Mustapha, Shomari Kapombe, Haji Mwinyi, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Himid Mao, Thomas Ulimwengu, Mudathir Yahya/Said Ndemla, Mbwana Samatta, Elius Maguli/Mrisho Ngassa, Farid Musa.

Algeria: M’bolhi Rais, Mandi Issa, Ghoulam Faouzi, Mesloub Wald, Medjani Carl, Zeffane Mehdi, Guediora Aldane, Taider Saphir/Belkarou Hichem, Belfodil Isha/Bentaleb Nabil, Slimani Islam, Mahrez Ryad.

No comments:

Post a Comment