Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Tuesday, October 1, 2024

Samatta kundini tena Stars

NAHODHA wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta amerejea kwenye kikosi cha timu hiyo kinachojiandaa na mechi za kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) nchini Morocco. Kwenye kikosi hicho kilichotangazwa jana na Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, jina la beki Novatus Dismas anayecheza soka la kulipwa Ulaya halimo kwa sababu ni majeruhi. Samatta anayeichezea PAOK ya Ugiriki, alikuwa miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha Stars kilichoshiriki fainali za Afcon 2023 zilizofanyika Ivory Coast, Januari na Februari, mwaka huu. Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Morocco alitaja wachezaji 23 akiwemo Samatta ambaye alijiweka kando. Morocco alisema kikosi cha Taifa Stars kitaingia kambini Oktoba 4, mwaka huu kujiandaa na michezo miwili ya kufuzu Afcon dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC) utakaochezwa Oktoba 10 na kurudiana Oktoba 15. “Kikosi kitaingia kambini Oktoba 4, mwaka huu na Oktoba 7 tutaondoka kwenda Lubumbashi, DRC kwa ajili ya mchezo wetu wa kufuzu Afcon utakaochezwa Oktoba 10,” alisema Morocco. Kuhusu Novatus alisema hajaitwa kwa sababu ya majeruhi na alimpa pole na kumtakia kila la heri apone haraka na kurejea kwenye majukumu yake. Kikosi cha wachezaji 23 cha Stars kinaundwa na makipa Ally Salim (Simba), Zuberi Foba (Azam) na Yona Amos (Pamba Jiji). Mabeki ni Mohamed Hussein (Simba), Lusajo Mwaikenda na Pascal Msindo (Azam), Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Ibrahim Hamad 'Bacca' (Yanga), Abdulrazack Hamza (Simba). Viungo kuna Haji Mnoga (Salford City, Uingereza), Adolf Mtasingwa (Azam), Habib Khaleed (Singida BS), Feisal Salum (Azam), Mudathir Yahya (Yanga) na Himid Mao (Tala'ea El Gaish SC, Misri). Washambuliaji ni Mbwana Samatta, Clement Mzize (Yanga), Kibu Denis (Simba), Nassoro Saadun (Azam), Abdullah Said (KMC), Selemani Mwalim (Fountain Gate) na Cyprian Kachwele (Vancouver Whitecaps, Canada).

No comments:

Post a Comment