Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Saturday, September 19, 2015

YANGA YATUMA SALAMU SIMBA BAADA YA KUIFUNGA JKT RUVU 4-1





MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga jana waliendelea kutoa dozi katika ligi hiyo baada ya kuwafunga maafande wa JKT Ruvu kwa mabao 4-1 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Ushindi huo ni kama inawatishia nyau wapinzani wao wa jadi Simba, ambayo itacheza nao mwishoni mwa wiki ijayo kwenye uwanja huo.

Huo ni mchezo wa tatu mfululizo kwa timu hiyo yenye maskani yake Jangwani kushinda na kuifanya kujikusanyia pointi tisa na mabao ya kufunga tisa huku ikiwa imefungwa bao moja tu hadi sasa.

Yanga walianza kwa kasi mchezo wao huo dhidi ya JKT Ruvu baada ya kulishambulia lango la wapinzani wao katika dakika ya kwanza tangu kuanza kwa mchezo huo, lakini Donald Ngoma alipiga shuti lililogonga mwamba na kurudi uwanjani baada ya pasi nzuri ya Niyonzima.

Katika dakika ya 21, Yanga nusura wafunge lakini shuti la Thaban Kamusoko la mpira wa adhabu liligonga mwamba na kutoka nje.

Baada ya kushambulia mfululizo, Yanga walifanikiwa kupata bao la kuongoza katika dakika ya 34, mfungaji akiwa ni Mzimbabwe Donald Ngoma  kwa shuti la mbali akimalizia pasi ya Amiss Tambwe.

Mrundi Tambwe aliifungia Yanga bao la pili katika dakika ya 47 baada ya kumalizia mpira uliotemwa na kipa wa JKT Ruvu.

Dakika mbili baadaye JKT Ruvu walijitutumua na kupata bao lililofungwa na Michael Aidan.

Tambwe aliendelea kuwa mwiba mchungu kwa maafande hao wa JKT Ruvu baada ya kufunga kwa kichwa bao la tatu katika dakika ya 62, akiunganisha wavuni kwa kichwa mpira wa kona iliyochongwa na Simon Msuva.

Msuva nusura aipatie Yanga bao la nne katika dakika ya 70 baada ya shuti lake akiwa ndani ya eneo la hatari kupanguliwa na kipa wa JKT Ruvu na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Kiungo mpya wa Yanga, Thabani Kamusoko aliifungia timu yake hiyo bao la nne na kuihakikishia kuondoka na pointi zote tatu baada ya kupiga shuti kali la mbali lililojaa wavuni.

Yanga: Ally Mustapha, Mbuyu Twitte, Haji Mwinyi, Kelvin Yondan, Nadir Haroub, Thaban kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/Salum Telela, Amiss Tambwe, Donald Ngoma/Malimi Busungu na Deus Kaseke, Geofrey Mwashiuya.

JKT Ruvu:Tony Kavishe, Michael Aidan, Napho Zuber, Martin Kazila, Madenge Ramadhani, George Minja, Ismail Azizi/Gaudence Mwaikimba, Naftali Nashon, Samuel Kamuntu/Abdul Mussa, Saady Kipanga/Emmanuel Pius na Mussa Juma.

Katika mechi zingine jana Jumamosi, Stand United iliifunga African Sports ya Tanga kwa mabao 2-0, Mgambo Shooting iliitambia Majimaji ya songea 1-0  na Prisons iliwatuliza ndugu zao wa Mbeya City kwa kuwafunga bao 1-0.

No comments:

Post a Comment