YANGA USO KWA USO NA KHARTOUM UWANJA WA TAIFA KESHO
Kuelekea katika mchezo huo unaotarajiwa kuwa wa vuta ni kuvute kufuatia timu ya Yanga SC kuhitaji ushindi katika mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuongoza kundi lake, huku pia Khartoum wakihitaji ushindi katika mchezo huo ili kuweza kuongoza kundi A.
Utamu wa mchezo huo unaletwa na makocha wa timu hizo mbili, Hans Van der Pluijm wa Yanga na James Kwesi Appiah wa Khartoum ambao wote wamewahi kufanya kazi nchini Ghana kwa vipindi tofauti.
Hans ambaye ametwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanznaia msimu huu, anasifika kwa kucheza soka safi la kasi na kushambulia muda wote, huku akiwa na mafanikiko nchini Ghana baada ya kuingia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na timu ya Berekum Chelsea miaka miwili iliyopita.
Kwa upande wa James Appiah alikuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Ghana, ambapo alikua kocha wa kwanza mwafrika kuipeleka timu ya Afrika katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Brazil mwaka 2014.
Licha ya kufuzu kwa fainali za kombe la Dunia, Appiah pia aliwahi kuichezea timu ya Taifa ya Ghana kwa miaka 7 akiwa nahodha, pia aliiwezesha timu ya Vijana ya Ghana chini ya miaka 23 kufuzu kwa fainali za Michezo ya Afrika na kutwaa Ubingwa huo mwaka 2011.
Katika kikosi chake cha Khartoum kinachoshiriki michuano ya Kagame, Appiah amejumuisha wachezaji wa kimataifa kutoka nchini Cameroon na Ghana, na malengo yake ni kutwaa Ubingwa wa Kagame Cup kwa mara ya kwanza.
Mpaka sasa Khartoum inaongoza kundi A ikiwa na pointi 7 sawa na Gor Mahia lakini Wasudani hao wakiwa juu kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa, huku Yanga wakishika nafasi ya tatu wakiwa na pointi sita.
Kabla ya mchezo huo kati ya Yanga SC dhidi ya Khartoum kutakua na mchezo wa kwanza utakaoanza majira ya saa 8 kamili mchana kati ya Gor Mahia ya Kenya dhidi ya Telecom ya Djibout.
Mpaka sasa timu zilizofuzu hatua ya robo fainali ni Khartoum, Gor Mahia na Yanga kutoka kundi A, huku APR na Al Shandy zikitoka kundi B, na Azam FC ikiwa timu ya kwanza kufuzu kutoka kundi C, na timu mbili kati ya Adama City, KCCA na Malakia zitaingia hatua ya robo ya fainali.
Hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la Kagame itachezwa Jumanne, Julai 28 na Jumatano Julai 29 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Post a Comment