KIKOSI cha Yanga kitawakosa nyota sita wa kikosi cha kwanza kitakapocheza mechi ya mwisho msimu huu dhidi ya wenyeji Ndanda FC katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara leo.
Wachezaji 18 wa Yanga waliondoka jijini hapa juzi saa nne asubuhi kwenda Mtwara huku nyota sita wa kikosi cha kwanza wakikosekana katika msafara huo kutokana na sababu mbalimbali ambazo zinaonekana kuwa neema kwa wapinzani wao, Ndanda FC ambao wanatakiwa kushinda mechi hiyo ili kuukwepa mstari wa kuiaga Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro, ameuambia mtandao huu kuwa kikosi chao cha Jumamosi kitawakosa nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye ni mgonjwa pamoja na winga hatari na kinara wa mabao VPL msimu huu, Simon Msuva, ambaye yuko nchini Afrika Kusini akifanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa.
Amewataja nyota wengine wanne ambao watakosa mechi hiyo kutokana na kuomba ruhusa ya kutokwenda Mtwara kuwa ni mchezaji ‘kiraka’, Mbuyu Twite (matatizo ya kifamilia) na kiungo Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ (ruhusa) pamoja na washambuliaji Mrisho Ngasa na Mliberia Kpah Sherman (ruhusa).
“Kikosi kimeondoka leo asubuhi bila nyota hao. Kombe litafuata baadaye na litabebwa na viongozi maana kwenye basi la wachezaji hakuna mahali pa kuliweka,” amesema.
Ndanda FC inayonolewa na meja mstaafu, Abdul Mingange, imekusanya pointi 28 katika mechi zote 25 zilizopita. Tayari kocha huyo na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Edmund Njowoka, wametamba timu yao itafia uwanjani kuhakikisha inaibuka na ushindi Jumamosi dhidi ya mabingwa hao mara 25 wa Tanzania Bara.
No comments:
Post a Comment