Jumamosi iliyopita, Terry, mwenye Miaka 35, aliichezea Chelsea Mechi yake ya 703 walipofungwa 3-2 na Sunderland huko Stadium of Light na kutolewa kwa Kadi Nyekundu na hivyo kufungiwa Mechi 2 badala ya moja ya kawaida kwa vile Msimu huu ashawahi kutolewa tena kwa Kadi Nyekundu.
Kifungo hiki kinamfanya Terry ashindwe tena kuichezea Chelsea Mechi zao 2 za mwisho za BPL, Ligi Kuu England, zilizobakia na hivyo kuifanya Mechi aliyocheza na Sunderland kuwa ndio ya mwisho kwake kwa vile Mkataba wake na Chelsea unakwisha mwishoni mwa Msimu huu.
Jumatano Chelsea wako Ugenini huko Anfield kucheza na Liverpool na Jumapili wanamaliza Msimu kwao Stamford Bridge kwa kucheza na Mabingwa wapya Leicester City na Terry hatakuwepo kuaga rasmi.
Ingawa mwenyewe Terry amesema wazi anataka abakie Chelsea lakini Klabu hiyo haijampa Mkataba mpya na habari za ndani za Klabu zimedokeza kuwa Meneja mpya anaechukua Timu kwa ajili ya Msimu ujao, Antonio Conte, ndie ameachiwa uamuzi wa kumbakisha Terry au la.
Licha ya kutokuwa na nafasi ya kuichezea tena Chelsea Msimu huu na pia kutokuwa na uhakika kama atakuwepo tena Stamford Bridge, Terry ameendelea kufanya Mazoezi na Timu kama ilivyotobolewa na Meneja Guus Hiddink ambae nae ndie anamaliza kazi.
Hiddink ameeleza: “Amefanya mazoezi na sisi na yupo poa. Ni wazi kutocheza kwake Mechi zetu mbili za mwisho ni pigo kwake na kwetu.”
No comments:
Post a Comment