WENYEJI Kenya, Harambee Stars wameanza vibaya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Ethiopia katika mchezo wa Kundi A, Uwanja wa Nyayo, Nairobi, Kenya.
Matokeo hayo yanaifanya Zanzibar iliyoshinda 2-1 mchezo wake wa kwanza dhidi ya Sudan Kusini iongoze Kundi na kujiweka katika mazingira mazuri ya kuingia Robo Fainali.
Ethiopia waliitesa Kenya kwa soka ya ‘Kibarcelona’, huku wachezaji wa Harambee wakitumia nguvu zaidi na maarifa haba.
Beki wa Ethiopia, Thok James akimdhibiti mshambuliaji wa Kenya, Allan Wanga leo Nyayo |
Allan Wanga alijaribu sana kuisumbua ngome ya Ethiopia, lakini bahati haikuwa yake jioni ya leo.
Kocha wa Kenya, Adel Amrouche Mbelgiji mwenye asili ya Algeria, hakuwepo kwenye benchi leo kuiongoza timu yake na habari zinasema amekerwa na kitendo cha wachezaji wake kutopewa posho kwa muda wote wa kuwa kambini kujiandaa na mashindano.
Kikosi cha Kenya kilikuwa; Duncan Ochieng, David Ochieng, Mussa Mohamed, Aboud Omar, Joackins Atudo/David King’atua k73, Peter Opiyo, Francis Kahata, Anthony Akumu, David Gateri, Edwin Lavatisa na Allan Wanga.
Ethiopia; Derete Alemu, Fasika Asfan, Salahadin Bargicho, Thok James, Moges Tedese, Shemeless Tegne, Mulualem Mesfin, Mintesnote Adane, Yussuf Yassin/Shimekit Gogsa dk89, Gebremichael Yakob/Yonathan Kebede dk46 na Foad Abbas/Manaye Fantu dk46.
Michuano hiyo itaendelea kesho kwa mechi mbili huko Machakos, Tanzania Bara ikimenyana na Zambia jioni baada ya Somalia na Burundi kupepetana mchana.
Kwa husani ya Bin Zubeiry
No comments:
Post a Comment