MILAN, Italia
KATIKA vitabu vya timu ya taifa
ya Italia ya wanaume, kuna majina ya wanasoka nguli waliopata kung’ara na
kikosi hicho, aidha kwenye michuano ya Ulaya ama fainali za dunia. Nyota kama Paolo Maldini,
Franco Baresi, Alessandro Del Piero na Francesco Totti, ni baadhi ya waasisi wa
soka kwa taifa la Italia na ulimwengu kwa ujumla.
Baada ya kizazi
cha kina Baresi, Maldini na Totti na kina Del Piero, ni muda wa kina Andre
Piero na kipa Gianiluig Gig Buffon ambao wako ukingoni mwa soka, kupigana kufa
kupona kuhakikisha wanafikia ‘level’ za magwiji waliopita.
Wakati kina
Maldin na nduguze wakiandikisha wasifu heshima, kwa upande mwingine kuna nyota
walioonekana kurithi fimbo zao, lakini ghafla hawakufikia malengo yao, kwa
sababu za hapa na pale.
Kwa msaada wa
mitandao ya kimataifa, Dimba, ilichambua nyota wa Kiitaliano ambao walipigiwa
upatu na wadau, wachambuzi wa masula ya soka, ambao pengine wangekuwa waasisi
wa taifa la kesho, ingawa ndoto zao zilipotelea kusikojulikana. Hii ni orodha
ya wanandinga hao.
Alberto
Aquilani
AS Roma, inaaminika
kwa kusaka, kukuza na kutunza vipaji vya wachezaji wazawa. Nyota kama Francesco
Totti na Daniele De Rossi, walikulia na kupatia umaarufu mkubwa wakiwa Roma. Alessandro
Florenzi katika kizazi kipya ndiye anatabiriwa kuwa lulu ya taifa kutoka klabu
ya Roma.
Ndivyo
ilivyokuwa msimu wa 2000 kwa Alberto Aquilani, alivyochipukia katika klabu ya
Roma. Kiwango chake kilizitoa udenda timu kubwa, zikiwemo Chelsea na Arsenal
zilizomtangazia ofa nzuri, lakini aliikacha ofa hiyo na kubaki Roma.
Aliiwezesha Roma kuweka rekodi ya kuchukua ubingwa wa
Serie A, mara mbili 2005 na 2006, rekodi iliyopitwa na Inter Milan baadaye-waliochukua
mara tatu. Pole pole Aquilani alianza kupotea katika ramani ya soka
kutokana na majeraha ya muda mrefu katika msimu wa 2006-07, lakini jeraha
alilopata msimu wa 2008-09, ndilo lilizima ndoto ya kufikia mafanikio ya kina
Totti na Del Piero.
Majeruhi aliyopata katika mechi ya Klabu bingwa Ulaya dhidi
ya Chelsea 2008, yalimuweka nje takribani msimu mzima, lakini alirejea uwanjani
baadaye, kabla ya Februari kupata jeraha jingine kubwa zaidi lililomuweka nje
msimu mzima.
Msimu 2009, Roma iliamua kumpiga bei kwa majogoo wa
Anfield, Liverpool, kwa uero mil. 20, kwa matarajio kuwa angekuwa mbadala wa
Xabi Alonso aliyetimkia Real Madrid, lakini hakuonekana uwanjani mpaka Novemba.
Visa na mikasa ilianzia hapo na hakuwa tena na uwezo wa
kucheza dakika 90 kama enzi zake pale Roma. Kuondoka kwa kocha Benitez, ndoto
ya Aquilani kupata namba kwenye kikosi cha kocha mpya, Roy Hodgson, zilikuwa
finyu na kuamua kumtoa kwa mkopo Juve.
Kidogo alipata
nafuu pale Juventus, ingawa hawakuwa tayari kumnunua. Kumalizika kwa mkopo huo, Liver ilimpeleka AC
Milan kwa mkopo tena, lakini janga la majeruhi liliendelea kumuandama tena.
Msimu uliopita, alijunga na Fiorentina ambapo kiwango
chake kidogo kirejee, lakini licha ya kuitwa kwenye timu ya taifa kwenye
michuano ya mabara mwaka huu, kiwango chake si kile jamii ya mpira ilitarajia
enzi za ujana wake na kamwe hawezi kufikia mafanikio ya kina Baresi.
Amauri
Mshambuliaji mwenye
asili ya Brazil, msimu wa 2007/8 alikuwa na nyota nzuri, baada ya kuifungia
Palermo mabao 15 kwenye Ligi kuu Serie A, kiwango kilichoanza kuzitoa mate vigogo. Ilikuwa ni Juventus, iliyomnasa kwa
kumfanya ‘swap’, dili-mbadilishano, kwa kuwapa Antonio Nocerino na kiasi cha
euro milioni 22.8.
Lakini pamoja na
upinzani wa namba Turin mbele ya wakali Alessandro Del Piero, David Trezeguet
na Vincenzo Iaquinta, bado Amauri alifunga jumla ya mabao 14, huku mabao mawili
akiyafunga kwenye mechi 10!
Pole pole, alianza kupotea msimu hadi msimu. Katika
msimu wa 2009/10, aliishia kuzifunga timu tano tu kati ya timu 30 alizokutana
nazo, huku msimu uliofuata akicheza mechi tisa na kushindwa kufunga bao hata
moja.
Ujio wa Antonio Conte kama kocha wa Juve, ndio kabisa
Amauri alikufa jumla. Alilazimika kupigwa bei kwa Fiorentina msimu wa
2011 kwa bei ‘ya nyanya’, euro 500,000, ikiwa na hasara ya uero mil. 22.3.
Amauri alitoa
mchango mkubwa kwa Fiorentina, bao la ushindi kwenye ushindi wa mabao 2-1 dhidi
ya AC Milan, lilitoa mwanya kwa Juve kutwaa ubingwa wa Serie A kwa kuwaacha
wapinzani, Milan pointi nyingi.
Imebaki kuwa historia kwa Amauri, kuwa aliwahi kuwa
kwenye kiwango kizuri, lakini kujiunga na Juve, ulikuwa mwanzo wa majanga, na
hana namba kwenye timu ya taifa tena. Msimu uliopita alifunga mabao 10 kwenye
mechi 33 alizoichezea Parma alipo kwa sasa.
Alberto
Gilardino
Akiwa na miaka 23, Alberto Gilardino alikuwa mmoja wa
nyota waliotikisa dunia, ikiwemo kuiwezesha Italia kutwaa ubingwa wa Dunia 2006. Hii leo
ana miaka 31, ameacha mshangao mkubwa kwa wadau wa soka.
Gilardino, alitikisa soka la Kiitalia, mabao yake 50
katika mechi 96 alizoichezea Parma tangu 2002/05, yaliwaumiza vichwa vigogo
nchini humo, na Rais wa AC Milan, Silvio Berlusconi, hakuwa na kigugumizi cha
kutoa euro mil. 25 kuhakikisha anachezea Milan.
Katika misimu yake mitatu pale Milan, Gilardino
alijijengea heshima kubwa kwa ufumaniaji wa nyavu, hasa katika michuano ya
Klabu bingwa Ulaya, ukiwemo msimu wa 2006-07, alipokuwa lulu ya ubingwa wa
UEFA. Ndiye aliizamisha Manchester United nusu fainali, kabla ya kuwapa ubingwa
Milan akitokea benchi na kufunga bao la
ushindi wa 2-1 dhidi ya Liverpool kwenye mechi ya fainali.
Pamoja na hayo, bado hakuwa Gilardino yule wa Parma,
msimu uliofuata 2008, alijiunga na Fiorentina kwa hasara ya euro mil.10.
Ulikuwa uhamisho wa maana kwake, alikutana na kocha wake wa zamani, Cesare
Prandelli, aliyekuwa kocha wa Parma, na msimu wake wa kwanza alifunga mabo 25
katika michuano yote.
Nyota ya mikosi ilianza kumuandama polepole, kuondoka kwa
Prendeli aliyejiunga na timu ya taifa, alipigwa bei kwa Genoa iliyokuwa daraja
la pili, kabla ya kuhamia Bologna msimu 2012 ambapo alifunga mabao 13 katika
mechi 36.
Lakini pamoja
na kushuka kiwango, ana kila sababu ya kumshukuru Prandelli, aliyempendelea
kwenye timu ya taifa. Bado anamthamini na alijumuisha kwenye kikosi
kilichoshiriki kombe la mabara na kumpa nafasi ya kuziba pengo la Mario
Balotelli baada ya kuumia.
Tangu awe na msimu mzuri na Parma wakati akiwa yosso,
Gilardino alitarajiwa kuwa tishio hata zaidi ya kina Baresi na Roberto, lakini
njia aliyopitia haikuwa ya mafanikio, na sasa ni babu asiyeweza kufanya cha
ajabu.
Antonio Cassano
Utukutu wa Antonio Cassano, si kigezo cha kuzima
kipaji chake. Cassano hana rekodi nzuri kwa klabu alizochezea, kutokana na
adhabu alizokumbana nazo.
Kizingiti cha kwanza ni alipokuwa na Roma, baada ya
kumbeza mwamuzi Roberto Rosetti wakati alipotolewa nje. Kitendo hicho
kiliwaudhi viongozi wa Roma na mwishowe kuuzwa Real Madrid msimu wa 2006 kwa
ada ya euro mil. 5, ikiwa ni hasara ya euro mil. 25, walizomnunua kutoka Bari.
Alipotua Real, alikumbana tena kocha Fabio Capello,
aliyetokea Roma na ‘kumpiga pini’ na baadaye kuamua kurejea Ligi ya Italia
kujiunga na Sampdoria kwa mkopo.
Ushirikiano wake na Giampaolo Pazzini waliiwezesha
Sampdoria kucheza Klabu bingwa Ulaya - moja ya mafanikio makubwa kwa timu hiyo.
Msimu wa 2010, alikumbana na kisanga kingine, baada ya
kuadhibiwa na Mwenyekiti wa Sampdoria, Riccardo Garrone, baada ya kukataa
kuhudhuria sherehe za tuzo. Cassano alifungiwa kucheza kikosi cha kwanza,
hivyo kuuzwa AC Milan msimu wa 2011.
Cassano, licha ya kuwa na kiwango kizuri msimu wa 2011/12,
alikumbana na matatizo ya kufanyiwa upasuaji wa moyo.
Kuondoka kwa Zlatan Ibrahimovic na Thiago Silva, naye
alivuka mitaa miwili, mitatu na kujiunga na Inter Milan kwa kubadilishana na
Giapolo Pazzini.
Utukutu wake umemfanya awe mtu wa kuhamahama, tayari
msimu huu amepelekwa Parma, haijawekwa wazi kama ‘alizikunja’ na Kocha wa Inter,
Andrea Stramaccioni, hadi kumuuza, lakini inahisiwa huenda kuna janga alitenda.
Hahami hivi hivi.
Ni matendo hayo, yamemfanya kushindwa kufikia mafanikio
ya kina Maldini, aidha kwenye klabu ama timu ya taifa, licha ya kuwa na kiwango
kizuri.
Fabio
Quagliarella
Baada ya kuapa kujituma mpaka apate namba kwenye kikosi
cha taifa, Fabio Quagliarella hatimaye ndoto yake ilitimia msimu wa 2006/7,
kufuatia mabao 13 aliyofunga akiwa na klabu ya Sampdoria msimu wa 2006-07.
Lakini uhamisho
wake kwenda Udinese, uligubikwa na utata mkubwa baina ya timu hizo, hata hivyo
ni Udinese ilishinda kesi hiyo. Katika misimu miwili, alifunga mabao 25 katika
michezo 73 na kuisaidia Udinese kufuzu kucheza Ligi ya Ulaya msimu wa '08-09.
Baadaye alihamia klabu ya nyumbani ya Napoli, lakini ujio
wa nyota wa Uruguay, Edinson Cavani kutoka San Paolo, alizima nyota ya
Quagliarella.
Ujio wa Cavani,
ulikuwa ni mwanzo wa kupotea kwa nyota huyo, kwani licha ya kuitwa kwenye
michuano ya dunia 2010 huko Afrika Kusini, hakupata nafasi, zaidi aliishia
kucheza dakika 45 tu kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Slovakia.
Licha ya Italia kushindwa kufuzu, lakini bao lake katika
mchezo na Slovakia, lilikuwa moja ya mabao matano ya michuano hiyo.
Kiwango ndani ya dakika 45 hizo, ziliwashawishi Juventus
kumchukua kwa mkopo. Aliifungia Juve mabao tisa ndani ya nusu msimu, lakini
maisha yalianza kuwa magumu baada ya kupatwa na jeraha la goti.
Kabla ya kupatwa na jeraha hilo, alitabiriwa kuwa nyota
mpya ya Italia ambaye angeweka rekodi kama wasisi waliopita, lakini majeraha ya
hapa na pale yamepelekea kutokuwa na namba kwenye kikosi cha taifa.
No comments:
Post a Comment