Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Wednesday, July 31, 2013

MASHINDANO YA MOSCOW KUWA MWISHO WA UFALME WA USAIN BOLT?

NDIYE mwanariadha mwenye kasi kuliko mwanariadha yeyote tangu kuanzishwa kwa mashindano ya riadha mwaka 1977. Sekunde 9.58, alizotumia katika mbio za mita 100, mwaka 2009 huko Berlin, unabaki kuwa muda mfupi katika vitabu vya Shirikisho la Riadha, IAAF.
Licha ya kushiriki mashindano mbalimbali, lakini rekodi hii inabaki kuwa ya kipekee. Katika mashindano ya Olimpiki ya 2012, Bolt aliahidi angeifikia kama si kuvunja kabisa rekodi hiyo, lakini hakufanikisha hilo, zaidi aliandikisha rekodi ya Olimpiki, kwa kutumia sekunde 9.63 katika mita 100.
Umaarufu wake umepambanua mpaka kwenye mbio fupi za mita 200 na zile za kukabidhiana vijiti 4×100m.
Kwa kifupi, tangu 2008, katika mashindano ambayo Bolt ameshiriki, medali za dhahabu zimepelekwa Jamaica. Na katika mashindano ya mwaka huu, gwiji huyo hakufanya makosa, alihakikisha medali za dhahabu zinapelekwa Jamaica, ikiwemo ya mbio za kukabidhiana kijiti.
Naam, huyo ndiye Usain St. Leo Bolt, miaka 26, mzaliwa wa Trelaway, Jamaica, ingawa baadae, aliamua kukimbia kijiji na kuhamia jijini Kingston.
Bolt, tayari amemaliza kazi aliyotumwa na taifa lake huko Uingereza-kurejesha heshima ya medali za dhahabu.
Kizingiti kimebaki kimoja tu, kuhakikisha anatetea heshima yake kwenye mashindano ya dunia yatakayoanza kutimua vumbi -Moscow Urusi Agosti 10-18. Mashindano ambayo yatawakosa wapinzani wakuu wa Bolt, Asafa Powell, Mjamaica mwenzake na Mmarekani Tyson Gay, waliofungiwa kwa tuhuma za kutumia dawa za kuongeza nguvu.
Gay, anashikilia nafasi ya tatu, nyuma ya Yohan Blake, kwa kuwa na rekodi ya kukimbia sekunde 9.71 huko Berlin Ujerumani, 2008 katika mashindano ya dunia mita 100. Huku Powell yeye anashika nafasi ya nne kwenye orodha hiyo ya ‘wakimbiza upepo’ maarufu duniani kwa rekodi ya kutumia  sekunde 9.72 Uswisi mwaka 2008.
Lakini licha ya kukosekana wakongwe hao (wote miaka 30), sio kigezo cha Bolt kutohofia upinzani, kwani kizazi kipya cha kina Yohan Blake kimekuja juu na lolote linaweza kutokea.
Hofu ya mashindano ya Moscow
Mashindano ya dunia yanatarajia kuanza kutimua vumbi mwezi ujao huko Moscow Urusi, ambapo tayari Bolt amethibitisha kuiwakilisha Jamaica kama si kutetea heshima yake. Lakini kigezo cha umri ambao kwa namna moja ama nyingine umeanza kumtupa mkono-miaka 26, kinaweza kuchukuliwa kama kigezo kikubwa cha gwiji huyo kushindwa kufurukuta mbele ya Yosso kina Blake (miaka 23) na Delano Williams (19).
Blake, kitendo cha kuvunja rekodi ya Gay, kinaashiria ni wakati wa damu changa na kusahau kile cha Tyson Gay, Asafa Powell, Olusoji Fasuba, na sasa Bolt taa zimeanza kuwaka kuashiria kufikia mwisho wa utawala.
Hivi karibuni Bolt alikiri kuwepo na upinzani mkubwa katika kizazi kipya, baada ya kushuhudia ‘dogo’ Delano Williams akifanya maajabu kwenye mashindano ya mita 200, huko Uingereza, pamoja na kutwaa medali ya dhahabu kwa vijana mwaka jana.
“Siachi kusema Williams atakuwa tishio duniani, maana ni mdogo na ni mpiganaji,” alisema Bolt.
Nguvu ya madawa
Imegundulika kuwa Bolt anatumia nguvu yake asilia, hivyo rekodi alizoandikisha katika tasnia hii, ni nguvu yake, tofauti na Gay na Powell ambao walidiriki kutumia njia za mkato kutafuta umaarufu.
Vipimo vilivyofanywa na Shirika la kupambana na utumizi wa madawa, USADA Mei mwaka huu, vilidhihirisha kuwepo kwa idadi kubwa ya wanariadha wanaotumia nguvu ya ziada huku idadi kubwa ikiwa ni Wajamaica.
Kuna kipindi alizushiwa kutumia madawa, lakini majibu ya vipimo vilivyochukuliwa wiki za hivi karibuni, vilibainika Bolt hatumii ‘nguvu ya ziada’.
Bolt na ufalme ya riadha
Pamoja na Gay na nduguze kutumia madawa ya nguvu za ziada, lakini hakuna aliyefanikisha kufikia rekodi ya gwiji huyu, labda Gay kidogo alijaribu kwa kutumia sekunde 9.75 mwaka huu huko Des Moines, Marekani.
Bolt, maarufu kama ‘Lighting Bolt’ mbali na rekodi hiyo ya mita 100, anashikilia rekodi ya kutwaa medali nyingi za dhahabu, ambapo ametwaa jumla ya medali 30, zikiwemo sita za mashindano ya dunia, tangu 2001 alipojiunga rasmi na mchezo huu.
Mwaka 2009, ulikuwa wa neema kwa Bolt pia, aliandikisha rekodi kwenye mbio za mita 200 kwa kutumia sekunde 19.19 Berlin Ujerumani, kabla ya 2012 kuwaongoza Yohan Blake, Michael Frater na Nesta Carter kuweka rekodi mpya kwenye mbio za kukabidhiana akijiti katika mashindano ya Olimpiki London-Uingereza 36.84.
Ni kwenye Olimpiki hizo, sekunde 9.63, zilimfanya Bolt kuandikisha rekodi mpya ya Olimpiki. Hiyo ilimfanya kushikilia rekodi zote za mchezo wa riadha kwa mbio fupi-Mashindano ya dunia na yale ya Olimpiki.
Swali linabaki je, Bolt ataweza kutetea medali zake huko Moscow? au ndio tuseme ni muda sasa wa damu changa ya kina Blake kumuondoa ‘mkoloni wa raidha’ ambaye amejitangaza kuwa mwasisi wa riadha muda wote.
Kifuta jasho: Powell alikuwa tishio kwa kutwaa medali za dhahabu wakati wa ujana wake kati ya miaka 21-25, vivyo hivyo kwa Gay, mpaka wanafungiwa wakiwa na miaka 30, hawakuwa na jipya, licha ya kusaidiwa na madawa kama inavyodaiwa. Picha inayojengeka kwa Bolt huenda asifurukute kwa Blake katika mashindano ya Moscow kutokana na umri.
Yetu macho, kwa hisani ya Supersport, tunangojea kwa hamu kumuona Bolt mbele ya Blake.
KUMBUKUMBU YA UWANJA
Mashindano ya mwaka huu yatafanyika kwenye dimba la Luzhniki Moscow, lenye  rekodi nzuri kwa mashabiki wa Man United, kwa kumbukumbu ya kutwaa kombe la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) dhidi ya Chelsea, kwa njia ya penalti. Juni 25, 2008 ni tarehe ambayo kamwe United hawawezi kuisahau, si kwa timu wala mashabiki tu, bali hata Kibabu Alex Ferguson (aliyekuwa kocha wake), kwani Luzhniki ndilo dimba la mwisho katika maisha yake ya soka, lililompatia ubingwa wa mwisho wa michuano hii, ikiwa ni mara ya tatu, akiwa kama kocha wa United ndani ya miaka 26 kabla ya kustaafu msimu uliopita.
Kwa upande mwingine, ni uwanja wenye chuki na watu Chelsea, hususan nahodha John Terry na aliyekuwa mshambuliaji wao, Nicolaus Anelka, walioshindwa kukwamisha nyavu zao na kuwapa ubingwa mahasimu zao. Dili la United kidogo ‘libumishwe’ na nyota wake, Cristiano Ronaldo, aliyekosa penalti ya tatu, lakini kushindwa kwa Terry kukwamisha mkwaju wa tano kwa Chelsea, ndio ulikuwa ukombozi wa Ferguson.

Wawakilishi wetu
Hakuna sura ngeni kwa upande wa  wawakilishi wa Tanzania, ni zile zile zilizoshiriki mashindano ya Olimpiki mwaka jana huko London, England. Faustine Mussa, Samson Ramadhani na Daudi Msenduki na msichana Zakia Mrisho, ndizo sura nne zinazotajwa kuliwakilisha taifa lenye idadi ya watu wapatao milioni 45, lakini pia huenda ikapungua kwa mujibu wa ripoti zilizopo. Ni idadi inayoshtua kidogo, ikilinganishwa na idadi ya taifa zima, ama kulinganisha na mataifa mengine yenye wawakilishi wengi.
Lakini cha kushangaza, pamoja na uchache huo, si wawakilishi labda pengine wanaweza kuwapa matumaini taifa kurejea na medali, kutokana na rekodi zao kwenye mashindano ya London. Tanzania iliishia kuwa kwenye vitabu vya ushiriki wa Olimpiki, kutokana na kwamba Mussa na Ramadhani walimaliza katika nafasi za mbali za 33 na 66, ambazo hii leo Mtanzania hawezi kujipa matumaini ya kurejea na medali. Vivyo hivyo kwa Mrisho, hali ilikuwa tete London pamoja na wawakilishi wa mchezo wa kuogelea na Seleman Kidunda kwa upande wa ngumi.
Ripoti zilizopo ni kwamba huenda Ramadhan asishiriki kutokana na kigezo cha umri kumtupa mkono, wakati Zakia, ambaye walau mashindano ya 2011 huko Daegu Korea Kusini alimaliza katika nafasi ya 11 kwenye mbio za mita 5,000, naye anaweza asiende ‘kwa kina Arshavin’ kupeperusha bendera. Dukuduku linabaki je, Tanzania haina vipaji vingine mpaka kuwakilishwa na watu wanne kati ya milioni 45?

No comments:

Post a Comment