KOCHA , Jose Mourinho amewasili tena kuinoa Chelsea ikiwa ni mara ya pili baada ya kuondoka katika timu hiyo miaka kadhaa iliyopita.
Kocha huyo ambaye ametokea kwenye timu ya Real Madrid safari hii atakutana na timu yenye vijana wengi na wenye vipaji ambao mmiliki wa timu hiyo, Roman Abramovich amewanunua baada ya kushindwa kuinua vipaji vya vijana katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa sasa timu hiyo ina wachezaji chipukizi kama vile, Nathan Chalobah, Nathan Ake, Jamal Blackman na Lucas Piazon ambao wanatajwa kuwa huenda wakawa wachezaji muhimu katika timu hiyo, ingawa wamekuwa hawatumiki.
Mbali na hao pia wapo wengine kama Oscar, Hazard na Azpilicueta ambao msimu uliopita waliweza kuonesha uwezo wao.
Pia wakati Courtois akikipiga kwa mkopo katika timu ya Atletico Madrid katika makala haya tunaangalia chipukizi wengine ambao mashabiki wa Chelsea wanatarajia msimu huu huenda wakambeba Kocha Jose Mourinho endapo atawatumia.
1. Marco van Ginkel
Kinda huyo ambaye anacheza nafasi ya kiungo mkabaji tayari ameshafikia uwezo wa kuchezea timu ya Taifa ya Uholanzi.
Akiwa na mwenzake Louis van Gaal, kinda huyo ndiye aliyeiwezesha timu ya vijana ya Uholanzi wenye umri chini ya miaka 21 kutwaa ubingwa wa Ulaya.
Inaelezwa kwamba kutokana na nguvu na kasi yake ndivyo vitakavyomuwezesha kupata namba katika kikosi cha Mourinho.
Mbali na hilo pia inaelezwa kuwa kutokana na kuwa Essien hayupo fiti na huku Oriol Romeu akiwa amepelekwa kwa mkopo jambo hilo linaweza kumfanya Mholanzi huyo kupata nafasi ya kuonesha uwezo wake msimu huu.
2. Andre Schurrle
Kinda huyo Mjerumani ambaye anakipiga pia kwenye timu ya taifa amesajiliwa msimu huu kwa pauni milioni 18 akitokea timu ya Bayer Leverkusen.
Hadi sasa mshambuliaji huyo wa pembeni ameshachezea timu ya Taifa ya Ujerumani mara 24 licha ya kuwa na umri mdogo jambo ambalo linadaiwa linaweza kumsaidia kama ilivyokuwa kwa mwenzake, Marko Marin.
Inaelezwa kuwa kinda huyo anaweza kucheza kama mshambuliaji wa pembeni ama kama mshambuliaji wa kati jambo ambalo linadaiwa Mourinho anaweza kumtumia mara kwa mara kulingana na mechi.
Kinda huyo nyota anadaiwa kuwa na kasi na mwenye mashuti ya nguvu jambo ambalo litamfanya kuwa hazina kwa kocha huyo.
3. Romelu Lukaku
Raia huyo wa Ubeligji aliutumia msimu uliopita akikipiga katika timu ya West Brom, ambako alifanikiwa kufunga mabao 17 katika mechi alizoichezea timu hiyo kwenye mashindano yote.
Msimu uliopita ndiyo wa kwanza kwa nyota huyo kucheza kwenye Ligi Kuu ya England baada ya kusugua benchi kwa muda mrefu ndani ya klabu hiyo.
Kutokana na nguvu na umbile lake ambalo limewafanya mashabiki wa timu hiyo kumpachika jina la Drogba mpya inasemekana Mourinho atamtumia mshambuliaji huyo kutokana na kwamba ndiyo wachezaji wa aina hiyo anaowapenda.
Inaelezwa kuwa licha ya Chelsea kuwa bado inahitaji kusajili washambuliaji wapya ingawa inao wengine kama kinda huyo Mbelgiji, Torres na Demba Ba, lakini itamlazimu, Mourinho kumtumia mshambuliaji mwenye nguvu ili aweze kumaliza msimu huu bila kuchanganyikiwa.
4. Kevin De Bruyne
Huyo pia ni mshambuliaji mwingingine raia wa Ubelgji ambaye aliutumia msimu uliopita akikipiga kwa mkopo ambaye anatajwa pia msimu huu anaweza kumbeba Mourinho.
Baada ya kuitumikia timu ya Werder Bremen na kufanikiwa kufunga mabao 10 na kusaidia kupatikana mengine 10 nyota huyo anaonekana kuwa ataweza kusimama vilivyo katika nafasi ya mshambuliaji wa pembeni.
Inaelezwa kuwa kutokana na uwezo aliounesha wa kuwasumbua wapinzani wake nyota huyo anaweza pia kufanya hivyo msimu huu akiwa na Chelsea.
Kutokana na kasi yake na uwezo wa kumliki mpira, De Bruyne anaweza kuifanya Chelsea kuwa tishio msimu ujao.
No comments:
Post a Comment