CHAMA ya Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA),
kimeipongeza timu ya Friends Rangers kwa kufuzu kucheza Ligi Daraja la Kwanza
msimu ujao baada ya jana Jumapili kuifunga Polisi Jamii ya mkoani Mara mabao
3-1.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 6 kwenye Uwanja wa
Karume mjini Musoma, Polisi waliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Katika mechi ya marudiano iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam
Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam na kuchezeshwa na mwamuzi Hans
Mabena kutoka Tanga, Rangers walipata mabao yao kupitia kwa Robert Katabi
katika dakika ya 53, Bakari Bakari dakika ya 67 na Mick Castro dakika ya 87.
Bao la Polisi lilifungwa na Faustine Faru katika dakika ya 68
na hivyo kuipa tiketi ya Friends Rangers kufuzu kucheza Daraja la Kwanza kwa
jumla ya mabao 3-2.
Ofisa Habari wa DRFA, Mohamed Mharizo, alisema ni faraja kwao
kuona Friends Rangers imetinga Ligi Daraja la Kwanza na kuuwakilisha vyema Mkoa
wa Dar es Salaam.
“Kwa niaba ya DRFA nachukua fursa hii kuwapongeza wachezaji,
viongozi na mashabiki wa Friends Rangers kwa uvumilivu na subra waliyokuwa nayo
katika kipindi chote cha ushiriki wa Ligi ya Mabingwa wa Mkoa, bado tupo pamoja
nao katika kufanikisha timu hiyo inafanya vizuri zaidi na hatimaye kucheza Ligi
Kuu Tanzania Bara,” alisema Mharizo.
Wawakilishi wengine kutoka Mkoa wa Dar es Salaam katika Ligi
ya Mabingwa wa Mikoa walikuwa Red Coast na Abajalo ambazo ziliaga michuano
katika hatua za awali.
No comments:
Post a Comment