Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Saturday, May 4, 2013

WAYNE ROONEY HANA MAISHA TENA NDANI YA OLD TRAFFORD



MANCHESTER, England
HAKUNA ubishi juu ya jambo hili, kwamba staa wa Manchester United, Wayne Rooney, hachezi kwa furaha tena Old Trafford, tofauti na ilivyokuwa miaka yake ya mwanzo wakati alipotua mahali hapo, ambaye hakuhitaji kutamka kwa mdomo, bali kwa kile alichokifanya ndani ya uwanja kilizungumza wazi.

Furaha ile ya utoto imetoweka na kubaki kuwa kumbukumbu tu, huku mara kadha ikishuhudiwa kwa siku za hivi karibuni kocha Sir Alex Ferguson, akiwa anamfanyia mabadiliko mchezaji huyo, hususani tukio la hivi karibuni katika mechi ya Ligi Kuu England pale Upton Park na alionekana kutokuwa na furaha sana katika kushangilia kunyakua ubingwa wa msimu huu, baada ya ushindi wao dhidi ya Aston Villa.

Rooney bado yupo  kwenye orodha ya wachezaji wenye viwango bora, katika hilo hakuna ubishi. Hata hivyo, kwa mchezaji mwenye umri wa miaka 27, hatuwezi kusahau kwamba anaingia kwenye kipindi muhimu zaidi cha maisha ya soka lake.
Lakini, badala yake amekuwa akihamishwa namba na kupangwa kwenye eneo ambalo hana uzoefu nalo, kiungo wa kati - kitu ambacho kimemfanya ashindwe kuonyesha ile kasi yake iliyokuwa ikiwatisha mabeki wengi wa timu pinzani na kuandika jina lake kwa muongo mmoja uliopita.

Kwa mara ya kwanza, wakati Rooney alipoibukia kwenye ulimwengu wa soka la kimataifa na kuwa mfungaji kijana zaidi kuwahi kufunga katika michuano ya Ulaya kwenye mechi dhidi ya Switzerland kwenye Euro 2004, kisha kutajwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Kulipwa miaka sita baadaye, mzaliwa huyo wa Croxteth, aliona kila kitu kinachohusu soka kipo miguuni mwake.

Lakini, kwa sasa mambo yamekuwa tofauti kabisa, fowadi huyo ambaye awali alikuwa akitajwa kwenye daraja moja la wakali kama Cristiano Ronaldo na Lionel Messi, kwa kipindi kile alichokuwa akifunga mabao, bila ya kusahau bao lake la kubinjuka alilowafunga Manchester City, Februari 2011, unaweza kuona kwanini staa huyo kwa sasa haonekani kuwa sawa.

Mambo kama hayo na mengine ndiyo yanayomfanya Rooney kujiona kama amevurugwa ndani ya United kwa sasa kutokana na nafasi anayopangwa kucheza.
Wenzake, Ronaldo na Messi wamezidi kupepea tu na kuonekana kama wamebaki wenyewe tu kwenye mbio za ubora tofauti na miaka kadha iliyopita, ambapo Rooney alikuwa miongoni mwao.
Weka kando suala la kushindana nao kifedha, kuchuana kimapato - lakini Rooney alionekana kuwa kwenye daraja moja na wakali hao, Messi na Ronaldo.

Inasikitisha kuona alivyo sasa Rooney, wakati mchezaji huyo ni mdogo kwa mwaka mmoja dhidi ya nyota mwenzake wa zamani wa United, Ronaldo, anayekipiga Real Madrid kwa sasa.
Sawa kwenye nafasi hiyo mpya, Rooney ameweza kuonyesha kiwango kizuri hasa ukizingatia pasi yake safi aliyompigia Robin van Persie na kufunga bao la aina yake katika mechi dhidi ya Aston Villa, lakini bado anaonekana mchezaji huyo hana furaha ya kucheza kwenye nafasi hiyo.

Ni wazi jambo hilo linamkwaza na hapendezwi na kitendo cha kucheza akiwa mbali na goli, kitu ambacho kwa sasa kinamfanya asitambulike tena kama mfungaji mahiri wa timu ya taifa ya England.
Kigezo cha kwanza kinachoonekana kwamba Rooney hayupo tayari kubeba majukumu yake hayo mapya ni namna alivyokuwa akipoteza mipira katika mechi dhidi ya Aston Villa, kilionekana kuwa kitu tofauti na alivyozoeleka mchezaji huyo mwanzoni alipoanza kucheza soka.

Jambo hilo liliibua maswali mengi, kwamba Rooney hapendezwi na majukumu mapya? Lakini, kuna kitu kimoja kinapaswa kufahamika hapa kwamba tofauti na alivyokuwa akicheza kwenye nafasi ya ushambuliaji, unapocheza kwenye kiungo na ukipoteza mpira basi kinachofuata ni kuadhibiwa na wapinzani.
Rooney atafanya makosa makubwa sana kama atamwaangalia nyota mwenzake, Ryan Giggs kama mfano wa mchezaji anayeendelea kuwa kwenye kiwango bora na hapotezi mipira kirahisi licha ya kuwa na umri wa miaka 39 kwa sasa.

Kinachotibua mambo ni kwamba mchezaji huyo kwa sasa anajiona yupo njia panda Old Trafford na kuwafanya mashabiki kuibua maswali ni nafasi gani kwa sasa atafiti mchezaji huyo.
Jibu lililo rahisi hapa ni kwamba kwa sasa hatapangwa tena kama mshambuliaji wa kati, kwa sababu nafasi hiyo tayari imeshachukuliwa na Mdachi Van Persie, ambaye amepewa jukumu hilo tangu alipojiunga na timu hiyo mwaka jana.

Van Persie bila shaka kwa sasa ni chaguo namba moja la Ferguson katika suala la mchambuliaji wa kati, hasa kama ilivyoonekana mara kadha kwamba Rooney amekuwa akitafutiwa nafasi nyingine kwa msimu huu.
Kitendo cha kuondoshwa katika kikosi kilichoanza kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya dhidi ya Real Madrid iliyofanyika Old Trafford, Machi kilikuwa na ujumbe mkubwa wa utanguzi juu ya nafasi yake kwa sasa kwenye kikosi hicho.

Kitendo hicho kilimuumiza sana mchezaji huyo, hasa ukizingatia ni hivi punde tu alikuwa akitajwa kuwa nyota muhimu wa kikosi hicho cha United.
Kwa mchezaji mwenye kiwango cha dunia kama Rooney, kuonekana nyongeza tu kwenye kikosi hasa ukizingatia Oktoba 2010, alisaini mkataba wa miaka mitano ya kubaki na timu hiyo, jambo hilo linamvuruga akili na kumwondoa katika moyo wa kimapambano wa kuisaidia timu kupata ushindi.

Wakati akitafahari hilo, kumekuwa na ripoti mbaya zaidi zinazoendelea kwenye vyombo vya habari kwamba United inafikiria kusajili washambuliaji wengine wa kati, Robert Lewandowski na Radamel Falcao, kitu ambacho kinaweka bayana kwamba Rooney hahesabiki tena kama fowadi.
Kwa hali ilivyo kwa sasa, bosi wa Rooney kwenye kikosi hicho cha United anaonekana hana mpango tena na mchezaji huyo na huenda wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa, mabingwa hao wa Ligi Kuu England watakuwa tayari kupokea ofa.

Tatizo lililopo ni kwamba Rooney anataka kuwa chaguo la kwanza la United katika safu ya ushambuliaji na katika hilo kama hatapewa uhakika basi anaweza kulazimisha kuihama timu hiyo mwishoni mwa msimu huu.
Klabu matajiri wa Ufaransa, Paris Saint-Germain, wanavumishwa kuwa na mpango wa kumvuta Rooney kwenye kikosi chao msimu ujao, kitu ambacho United inaweza kuketi mezani na kumwaachia mchezaji huyo kama mabingwa hao wa Ligue 1 watakuwa tayari kulipa pauni milioni 40 na kukidhi matakwa na mchezaji mwenyewe.

Kabla ya kusaini mkataba mpya Oktoba 2010, Rooney alitishia kwamba angekwenda kujiunga na mahasimu wa United, Manchester City - lakini Ferguson aliishinda vita hiyo na sasa anaonekana hana mpango wa kutaka kuendelea na huduma ya mshambuliaji huyo wa Three Lions.

Kama hatatumika kama mshambuliaji wa kati, je, Rooney ataendelea kubaki United na kucheza maisha yake yote kama kiungo? Usicheze kamari kwa vyovyote kwenye hili au hata kuamini kama Rooney ataendelea kubaki hapo hadi msimu ujao.

No comments:

Post a Comment