Beki wa Ashanti (mwenye jezi nyekundu ) akiondoa mpira kwenye himaya ya mshambuliaji wa Villa Squad kwenye mchezo wa lligi daraja la kwanza uliochezwa uwanja wa Karume jijini Dar es salaam |
TIMU ya Ashanti United imekata tiketi ya kucheza Ligi Kuu
msimu ujao baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Villa Squad kwenye mchezo wa
Ligi daraja la kwanza uliochezwa uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam juzi.
Kwa matokeo hayo Ashanti imefikisha pointi 28 ambazo
haziwezi kufikiwa na timu yoyote kwenye kundi B hata wakifungwa michezo miwili iliyosalia
huku Villa wao wakiwa na pointi 20 na michezo miwili pia.
Mchezo huo ulikuwa na ushindani mkubwa na uliojaa ufundi huku
mashabiki wa timu zote wakichangia kasi ya uchezaji kutokana na kushangilia
kuanzia dakika ya kwanza hadi ya 90.
Ashanti walijipatia bao dakika ya tisa kupitia kwa Zablon
Raymond wa Villa ambaye alijifunga wakati akiokoa shuti la Maliki Jaffary kwa
kichwa na kutinga wavuni, Villa walisawazisha bao kupitia kwa Ali Mrisho baada
ya kuwazidi mbio mabeki wa Ashanti na kufanya timu ziende mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
Kipindi cha Pili kwa timu zote kuendelea kushambulia na
kufanya mabadiliko na dakika ya 54 mshambuliaji Fakii Rashid wa Ashanti
aliwanyanyua mashabiki baada ya kuwapiga chenga mabeki wa Villa na kubaki na
golikipa na kufunga bao kirahisi lakini Villa nao walizidisha mashambulizi na
dakika ya 65 walisawazisha bao kupitia kwa Amri Mwideni baada ya kutokea piga
nikupige langoni kwa Ashanti.
Kwa matokeo hayo ambayo yamepokelewa kwa furaha na mashabiki
na viongozi, Ashanti imeungana na Mbeya City ambayo ipo kundi A kukata tiketi
ya kucheza ligi kuu msimu ujao na kuliacha kundi C ambalo ni gumu wakiwania
nafasi moja ambapo timu za Rhino, JKT Kanembwa na Pamba mojawapo anaweza kuichukua endapo yeyote
atafanya vibaya.
Mchezo mwingine kwenye kundi B umechezwa kwenye uwanja wa
Mabatini, Pwani na Polisi Dar es Salaam wakaifunga Green Warriors mabao 2-1.
Kundi C ilichezwa michezo minne, mkoani Mara maafande wa
Polisi Mara waliifunga Polisi Dodoma bao 1-0 mchezo uliochezwa uwanja wa Karume, uwanja wa
Kambarage Shinyanga Rhino Rangers ya Tabora waliondoka na pointi tatu baada ya
kuifunga Mwadui bao 1-0.
Kwenye uwanja wa Lake Tanganyika wenyeji JKT Kanembwa waliifunga
Polisi Tabora mabao 2-0 na mjini Kiteto Manyara, Pamba na Morani walitoka sare
ya 0-0
Kundi A, Kurugenzi ya Makambako
iliutumia vema uwanja wa nyumbani na kuweza kuwafunga vinara wa kundi hilo
ambayo imekwisha kukata tiketi ya kucheza ligi kuu msimu ujao, Mbeya City bao 1-0 .
No comments:
Post a Comment