TIMU ya Tanzania
itakayoshiriki Michezo ya 33 ya Olimpiki Paris, Ufaransa imeagwa na kusema wako
tayari kuitetea bendera ya taifa.
Akizungumza katika
hafla ya kuiaga timu hiyo Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam jana, nahodha
Alphonce Simbu alisema wamejiandaa vizuri na wako tayari kwa mapambano.
Alisema anajua Michezo
ya Olimpiki ni migumu na inashirikisha nyota na magwiji wa riadha duniani ila
wamejipanga kuweka historia kwa kurudi na medali.
"Huu ni mwaka
wetu, maandalizi tuliyofanya hakuna shaka tutakuwepo ndani ya tatu bora, mwaka
huu Tanzania itafanya vizuri,” alisema Simbu.
Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Suleiman Serera aliwataka wachezaji
hao kwenda kupambana kwani wameandaliwa vizuri.
"Rais Samia
Suluhu Hassan ametutuma tuwaeleze kuwa atafuatilia mashindano yenu, nchi iko
pamoja na ninyi na serikali itawagharamia posho zenu ili mwende Paris bila
mawazo," alisema.
Alitaka mashirikisho
na vyama vya michezo kuanza maandalizi mapema kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki
ya 34 itakayofanyika Los Angeles, Marekani 2028.
Hata hivyo, Dk Serera
amewashauri wanamichezo kujitunza akimtolea mfano Simbu ambaye alisema mwaka
2015 yeye Serera akiwa masomoni, Beijing China mwanariadha huyo alikuwa
anatamba na hadi sasa bado anafanya vizuri.
Mkuu wa msafara kwenye
michezo hiyo, Henry Tandau alisema safari ya timu imekamilika na kwenye
ufunguzi bendera ya Tanzania itabebwa na Sophia Latiff na Andrew Mlugu.
"Nahodha (Simbu)
kwenye ufunguzi atakuwa hajawasili Paris,” alisema Tandau.
Wachezaji wanaounda
timu hiyo ni waogeleaji Collins Saliboko na Sophia, mcheza judo Mlugu na
wanariadha, Jackline Sakilu, Magdalena Shauri, Simbu na Gabriel Geay wote
wanakimbia marathoni.
Wengine katika msafara
huo ni makocha, Anthony Mwingereza (riadha), Alex Mwaipasi (kuogelea) na
Innocent Mallya (judo) watakaoambatana na mkuu wa msafara Henry Tandau, mwandishi
wa habari Muhidin Michuzi na daktari wa timu, Eliasa Mkongo.
Tanzania hadi sasa
haijawahi kutwaa medali katika Michezo ya Olimpiki tangu mwaka 1980 wakati
Filbert Bayi na Suleiman Nyambui waliposhinda medali za fedha za meta 3,000
kuruka gogo na maji na meta 5,000.
No comments:
Post a Comment