TANZANIA imepanda nafasi moja katika viwango vya ubora wa soka kutoka nafasi ya 114 hadi 113 katika viwango vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) vilivyotolewa jana.
Huo ni mwendelezo
mzuri wa timu ya soka ya Taifa kufanya vizuri kwenye michezo yake kwani Mei mwaka
huu ilipanda tena kwa nafasi nne kutoka 119 (Februari) hadi 115 ambavyo vilitolewa
Mei mwaka huu.
Tanzania imepata pointi
1,175 sawa na mwezi uliopita baada ya Taifa Stars kucheza na Zambia mchezo wa
kufuzu Kombe la Dunia 2026 jijini Ndola na kushinda kwa bao 1-0.
Kwa upande wa nchi
za Afrika Mashariki, Uganda imeshuka kwa nafasi moja, sasa ipo 96 kutoka 95 na
Kenya imeendelea kubaki 108 licha ya kucheza michezo mitatu na kushinda miwili
na kufungwa mmoja.
Kwa upande wa
Afrika, Morocco imeendelea kushikilia usukani licha ya kushuka kwa nafasi mbili
kwenye viwango vya dunia huku nafasi ya pili ikikamatwa na Senegal na nafasi ya
tatu ni Misri.
Argentina
imeendelea kushika nafasi ya kwanza duniani ikifuatiwa na Ufaransa na Hispania
ya tatu ikiwa imepanda kwa nafasi tano, England inashika nafasi ya nne na
Brazil inashika nafasi ya tano.
No comments:
Post a Comment