|
Red Arrows |
|
Kikosi cha APR |
TIMU za APR ya Rwanda na Red Arrows ya Zambia leo zinatarajiwa kucheza
fainali ya Kombe la Dar Port Kagame 2024 kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam,
Tanzania.
Mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu utakuwa kati ya Al Hilal dhidi ya Al
Wadi zote kutoka Sudan.
Timu ya APR inayofundishwa na kocha Darko Novic iliiondoa Al Hilal kwa
mikwaju ya penalti 5-4 katika nusu fainali ya kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja
wa KMC na Red Arrows ikaifunga Al Wadi FC ya Sudan kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja
wa Azam Complex, Chamazi juzi.
APR ambao wameshinda kombe hilo mara tatu walifuzu fainali bila kupoteza
mchezo tangu hatua ya makundi lakini mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Zambia
walipokea kichapo cha mabao 5-0 kutoka kwa Al Hilal katika mechi za makundi.
Kocha wa APR, Novic alisema anajivunia wachezaji wake ambao wana ari ya
kupambana tangu mwanzo hadi kufuzu kwa fainali.
"Bado tuna kazi kubwa ya kufanya kwa sababu maandalizi ya fainali ni
tofauti hasa baada ya kucheza dakika 120 katika nusu fainali," alisema
Novic.
Naye mchezaji wa Red Arrows, Allasane Diarra ambaye alinyakua tuzo ya
mchezaji bora wa mechi alisema hawakukata tamaa tangu mwanzo hadi mwisho.
"Hii haikuwa mechi rahisi, lakini tulicheza kwa mioyo yetu na kufika
fainali," alisema Diarra.
Katika
michuano hiyo ambayo itamalizika leo, mabingwa watajinyakulia zawadi ya fedha
taslimu dola za Marekani 30,000 (Sh milioni 78), mshindi wa pili dola za
Marekani 20,000 (Sh milioni 52) na mshindi wa tatu dola za Marekani 10,000 (Sh
milioni 26).
No comments:
Post a Comment