MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imekubali ombi la Klabu ya Yanga la kusogezwa mbele kwa muda wa kusikilizwa kesi iliyofunguliwa na wanachama wa klabu hiyo kuhusu uhalali wa Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo.
Awali mahakama hiyo
iliamuru Uongozi wa Yanga ukiongozwa na Rais Hersi Saidi kuachia ngazi kwa kile
kilichodaiwa kuwa Katiba ya Yanga haitambui uwepo wao.
Kufuatia hatua hiyo mahakama hiyo imewapa siku
14 kama walivyoomba Yanga kufanya mapitio kisha kesi itasikilizwa upya kukiwa
na pande zote mbili.
Hivi karibuni Yanga walipokea hukumu ya kutotambulika kwa Baraza la Wadhamini la klabu
hiyo kutokana na hukumu iliyotolewa Agosti 2, 2023 na Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu.
Mkurugenzi wa Sheria wa Yanga, Wakili Simon Patrick
alisema Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ilisikiliza kesi hiyo
iliyofunguliwa na Juma Ali na Geofrey Mwaipopo upande mmoja kwani klabu
haikushirikishwa.
Alisema Abeid aliwasilisha utetezi ambao saini za
klabu zilighushiwa akidai wamemteua kwenye kesi hiyo mbele ya Hakimu Mwandamizi
Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Pamela Mazengo.
Alisema Juma Ali na Geofrey Mwaipopo ambao walikuwa
upande wa walalamikaji na Juma Abeid alikuwa upande wa Yanga (walalamikiwa)
alikuwa akikubali kila kitu kilichokuwa kinaombwa na upande wa walalamikaji.
Baada ya hapo jopo la wanasheria wa Yanga walipeleka
maombi mahakamani kuomba kuongezewa muda kwa ajili ya kufanya mapitio kwani
muda wa kukata rufaa umeshapita na kukubaliwa.
Hukumu hiyo ilitokana na kesi ya msingi iliyofunguliwa
Agosti 4, 2022 na walalamikaji Ally na Mwaipopo wakitaka kutotambulika kwa
Baraza la Wadhamini la Yanga lililowekwa madarakani kwa katiba ya mwaka 2010,
kukosa sifa kisheria.
Aidha, walalamikaji pia walitaka miamala yote ya fedha
iliyoidhinishwa na baraza hilo, kutotambulika kisheria kwa kuwa ni batili.
Hukumu hiyo imeitaka bodi iliyokuwa madarakani kwa
katiba ya mwaka 1968 iliyofanyiwa mabadiliko mwaka 2011, kurudi madarakani
kuongoza klabu ya Yanga.
Inaelezwa kuwa walalamikaji walirudi mahakamani
kukazia hukumu hiyo kuiondoa madarakani bodi hiyo ya wadhamini ndipo uongozi wa
sasa wa Yanga ukapenyezewa taarifa.
Baraza lililolamikiwa linaongozwa na Mwenyekiti George
Mkuchika na wajumbe ni mama Fatma Karume, Dk Mwigulu Nchemba, Tarimba Abbas na
Antony Mavunde.
No comments:
Post a Comment