Na Rahel Pallangyo
WAKATI wa safari yangu ya Tanga hivi karibuni katika
michuano ya Ngao ya Jamii kwenda kuandika habari na kupiga picha za michezo,
nilipita karibu kabisa na jumba la sinema la Majestic lililopo barabara ya
Mkwakwani.
Jumba hilo la Shirika la Nyumba (NHC) ni la zamani na mpaka
sasa linaendelea kuonesha filamu na kufanya kazi nyingine za burudani.
Ikumbukwe kuwa katika miaka ya 1980 ambako kulikuwa na mdororo wa kiuchumi hamu
ya kwenda sinema ilipungua kutokana na majumba hayo kutokuwa na bidhaa mpya
inayovutia wakawa wanababia na kuchosha wapenzi wa sinema. Katika jengo hilo
Tanga wapenzi wa sinema wanaopenda kuona vitu hivyo katika ‘Big Screen’
walipoteza burudani hiyo kutokana na kufungwa kwa majumba ya sinema ambayo
yalikuwa na uwezo wa kuonesha mm 35 bado wanaendelea kuona kwa kutumia jengo
lao ambalo ujenzi wake ni urithi safi wenye kumbukumbu. Ingawa wapenzi wa
burudani hiyo kabla ya miaka ya 1980 hawakuweza kufikiri hata mara moja kwamba
kutakuwa na kufungwa kwa majumba ya sinema ukizingatia wananchi walikuwa
wanafurika kuona sinema za kidosi au za kizungu. Mathalani Dar es Salaam
majumba yote yaliyokuwa yakionesha filamu kama Drive in, Empire, Avalon,
Empress, Odeon, Cameo, New Chox na Star Light yamegeuka kuwa majumba ya kazi
nyingine na mpaka kesho inaonekana haiwezekani tena kurejea katika mazingira ya
zamani. Ukiachia Dar es Salaam mji wenye starehe za kipekee wa Morogoro ulikuwa
na Shani Cinema na Sapna. Vivyo hivyo katika Mkoa wa Lindi ambapo pale penye
ukumbi unaoitwa Y2K kulikuwa na jengo kubwa la filamu. Mpaka mwishoni mwa miaka
ya 1990 ilikuwa ni ada kutafuta magazeti kuona nini kinaendelea katika majumba
ya sinema ya Dar es Salaam na hata huko mikoani katika mbao za matangazo ya
majumba hayo. Ingawa majumba mengi yamekuwa nyumba za ibada, maduka au
yamefungwa au kubomolewa na majengo mengine kusimamishwa badala yake, Tanga
wameonesha kwamba Majestic yao ambayo ilitumika kuonesha filamu ya kwanza huru,
Shamba Kubwa, inaweza kuendelea kuwapo. Majestic Theatre haikuwa peke yake
katika mji huu ambao kuingia ni rahisi na kutoka ni kazi kwani kulikuwa na
Regal, Novelty na Tanga Cinema lakini leo hii unaona kwamba Majestic ndio
wameendelea kuwapo mpaka kesho na bado wanaonesha inawezekana kuendelea
kuonesha filamu. Historia inasema katika Jiji hilo jengo la kwanza kufa ni
Tanga cinema, ikafuata Novelty, Regal na mwisho Majestic ambao kwa sasa
wamefufuka. Nilipata nafasi ya kuzungumza na mmoja wa walimu wa sanaa ya
filamu, Profesa Martin Mhando kuhusiana na jengo la Tanga na kuniambia ndilo
lililotumika kuonesha filamu ya kwanza huru ya Shamba Kubwa ambayo pia ploti
yake ilikuwa Mkoa wa Tanga. Aliniambia ingawa Majestic ya Tanga haina uhusiano
na jengo la jina kama hilo Zanzibar ambalo lilipiganiwa kuimarishwa na
kuendelea na kazi yake ya kuonesha filamu, anaamini utamaduni wa kuona sinema
unarejea kutokana na juhudi mbalimbali za watengeneza filamu hapa nchini na
duniani kwa ujumla. Shamba Kubwa moja ya filamu zilizoanzisha tena utengenezaji
wa filamu Tanzania baada ya kampuni ya filamu kufa na filamu zake kubaki
Zimbabwe zilipoenda kwa ‘treatment’. Shamba Kubwa sinema ya mwaka 1994
ilimtambulisha Jimmy Mponda kama J. Plus wengine wakimuita Jimmy Master ilipata
jina kubwa na pia kuleta vuguvugu mpya ya matamanio ya burudani kupitia majumba
ya sinema. “Majestic Theatre ya Tanga naijua kama moja ya majumba ambayo
yalibaki kuonesha filamu kwa muda mrefu wakati majumba mengine yalipokufa
kabisa Tanzania. Mwaka 1995 ilipotengenezwa Bongo Movie ya kwanza iliyoitwa
“Shamba Kubwa” na Amri Bawji na Kassim El Siagi, filamu hiyo ilioneshwa
Majestic, Tanga,” anasema Profesa Mhando na kusema kuwa hali iliyokuta majumba
ya sinema nchini Tanzania Bara na Visiwani matokeo ya mdororo wa kiuchumi. “Uchumi
ulidorora miaka ya 1980,” Mhando alisema. “Tiketi zilikuwa zimegharimu dola za
Marekani 1-2, lakini tulijua ikifika dola 3 uchumi wa sinema utaporomoka na
ndivyo ilivyokuwa. Watu hawakuwa na uwezo wa kutazama sinema. Video zilikuja na
kukaa ndani. Kufikia 1996, sinema zote zilikuwa zimefungwa.” Anasema ingawa
hana uhakika kuwa Majestic ya Tanga na Majestic Zanzibar zilihusiana ingawa
inawezekana, maana waliokuwa wanahodhi majumba ya sinema walikuwa Watanzania
wenye asili ya India, kuendelea kuwepo kwa jengo hilo likiendelea na kazi ya
kuleta burudani inatia matumaini si tu kwa urithi wa kizazi kijacho bali na
uhakika wa maeneo ya kuonesha uwezo wa binadamu katika skrini kubwa. Anasema
alikuwa anapigania sana Majestic ya Zanzibar na anafikiria safari ni nzuri kwa
kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa tayari kulifufua Jumba la Majestic
kwa kupata misaada ya kimataifa. “Mimi nimekuwa nikipigia kelele na kuliwekea
kifua ili lisibadilishiwe matumizi kama majumba mengine. Kwa sasa jumba hilo
limetolewa kwa Muungano wa taasisi tano kusimamia ukarabati na kulipa matumizi
mengi zaidi,” anasema Profesa huyo ambaye amebobea katika filamu. Taasisi hizo
tano ni ZIFF, Hifadhi, Sauti za Busara, Women Reclaim Center na Abdul Mawazo.
Anasema Unesco imesaidia kupata kiasi cha fedha toka serikali ya Japan ili
kufanya upembuzi yakinifu na kuanza mipango ya kukarabati jumba hilo. Ingawa
kuna utata katika uhodhi/umiliki wa jumba lenyewe maana nalo lilitaifishwa
wakati wa mapinduzi na sasa familia iliyokuwa inalimiliki imerudi tena ili
kutaka kuliendesha, mazungumzo yanaendelea kuhusu umiliki na hivyo kazi ya
upembuzi imesimama. Unesco ndiyo inasimamia ukarabati. Hekaheka za kurejesha
jumba hilo la Zanzibar linaenda na ukweli kuwa majumba ya sinema katika miaka
ijayo ni muhimu katika kuhakikisha ukuaji mzuri wa tasnia kwani hata Ulaya
walikoendelea bado majumba ya sinema yanafanyakazi hasa kuwezesha pato la
kwanza katika kuingia katika majukwaa mengine. Majestic ya Zanzibar ni moja ya
majumba ya kwanza ya sinema barani Afrika, katika miaka ya 1920. Zanzibar
ilikuwa na majengo ya sinema 53 yakajifia na kubaki mawili likiwemo hilo la
Majestic. Mtengenezaji wa filamu Mwingereza Nick Broomfield, anayejulikana kwa
filamu za Biggie na Tupac, Aileen Wuornos: The Selling of a Serial Killer na
Battle For Haditha anafurahishwa na juhudi za kurejeshwa kwa majumba ya sinema.
Akizungumzia jumba la Zanzibar ambalo halina paa kwa sasa watu wakiangalia
sinema wazi alisema: “Ingawa sinema haina paa, watu wanaitumia na kuweka
projekta yao wenyewe. Pengine ina kumbukumbu nyingi kwao. Ni mahali ambapo watu
walienda kwa kustarehe na kukutana na rafiki zao wa kike wa kwanza. “Sinema ni
uzoefu wa pamoja. Kama mtengenezaji wa filamu, jambo la ajabu zaidi kuhusu
kutazama na kikundi cha watu ni kwamba unaweza kujua ni sehemu gani za filamu
zinafanya kazi na zipi hazifanyi kazi. “Ni jambo la kuunganisha, njia ya
kufanya kikundi au eneo pamoja. Nilipokuwa mdogo, kila mtu alienda kwenye
sinema Jumamosi asubuhi ili kuona katuni. Ilikuwa ni ushirikiano wa kijamii, na
hiyo ni moja ya mambo ya kusisimua ambayo yanaweza kutokea. “ Broomfield
anasema: “The Majestic ni kipande cha usanifu wa ajabu ... Kwa upande wa
jumuiya ya watengenezaji filamu wa Afrika Mashariki, umuhimu wa Zanzibar
ungewekwa katika kufufua Majestic. Ingekuwa faraja kwa watu kuchukua sinema kwa
uzito. Pia itakuwa vyema kwa tamasha la filamu la Kimataifa la Zanzibar.”
“Nadhani ikiwa ingerekebishwa ipasavyo, watu wangeweza kwenda kwenye sinema
huko mara kwa mara. Bado ina mapambo mazuri ya sanaa.” Mmoja wa wapenzi wa
sinema Beda Msimbe anasema ana tumaini kizazi kipya kikionja ladha ya kuingia
majumba makubwa na utamaduni wake wataona raha. “Wazee bado wana ndoto zao za
kutazama sinema kila wiki, wanakumbuka utukufu wa zamani wa majumba haya na enzi
za ujana wao. Huo ndio umuhimu wa utamaduni wa sinema kwao.” Majestic ya Tanga
hivi karibuni ilionesha filamu ya kisayansi ya Eonii na mhudumu wa jumba hilo
anasema walijaza watu wa rika zote na kutamani hali hiyo kuendelea kuwa hivyo.
No comments:
Post a Comment