Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Pindi Chana |
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Said Yakubu |
Kikundi cha ngoma kutoka Mkoa wa Kilimanjaro kikitumbuiza |
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalum, Kapteni Mstaafu George Mkuchika ameiasa jamii kuenzi mila na desturi za Tanzania ambazo ndio utambulisho wa Taifa hilo ndani na nje ya nchi, na kuacha kuiga utamaduni usiofaa wa Mataifa mengine.
Mkuchika amesema hayo Agosti 27, 2023 Mkoani Njombe, alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kufunga Tamasha la pili la Utamaduni lililokua na Kauli Mbiu 'Utamaduni ni Msingi wa Maadili Tuulinde na Kuendeleza'
"Nawapongeza kwa kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo yanaenzi maono ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1962 alipozindua Wizara ya Vijana na Utamaduni ambapo alisema Taifa lisilokua na Utamaduni wake ni Taifa Mfu na ni sawa na mwili bila nguo" Mhe. Kapt Mstaafu George Mkuchika
Naye Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Pindi Chana amesema, lengo la tamasha hilo ni kutoa fursa kwa Watanzania kuufahamu Utamaduni wa Tanzania kuusherehekea, kuutunza, na kuuendeleza utamaduni wao pamoja na kubadilishana utamaduni wa mkoa mmoja na mwingine.
Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu amesema katika tamasha hilo, shughuli mbalimbali zimefanyika ikiwemo shindano la kuibua vipaji la Njombe Vibe, mbio za polepole, mashindano ya vyakula na ngoma za asili, maonesho ya shughuli za utamaduni na sanaa, mdahalo wa kukabiliana na mmomonyoko wa maadili pamoja maonesho ya filamu ya The Royal Tour katika kuunga mkono jitihada za Rais Dk Samia Suluhu Hassan, za kuitangaza Tanzania.
Katika Tamasha hilo Mkoa wa Mwanza umeibuka mshindi wa kwanza wa ngoma za asili ukifuatiwa na Dodoma na namba tatu ni Mkoa wa Njombe, ambapo pia katika mashindano ya vyakula vya asili Mkoa wa Kilimanjaro umeibuka Mshindi ukifuatiwa na Iringa.
Katika hatua nyingine Tamasha la tatu la Utamaduni Kitaifa mwaka 2024, litafanyika katika Mkoa wa Morogoro Agosti 24-26 ambapo mkoa huo umesisitizwa kujiandaa vyema.
No comments:
Post a Comment