MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu bara, Yanga leo imeduwazwa na
Lipuli baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1
katika mechi yake ya kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Matokeo hayo hayakutarajiwa na wengi kutokana na ugeni wa
Lipuli kwenye ligi na hivyo iliingia uwanjani ikiwa haipewi nafasi ya kushinda.
Lipuli iliyopanda Ligi Kuu msimu huu, ilikuwa ya kwanza
kupata bao katika dakika ya 45 kupitia kwa Seif Abdallah akiunganisha pasi ya
Malimi Busungu kabla ya kuachia shuti lililojaa wavuni.
Dakika tatu za nyongeza ziliitosha Yanga kusawazisha bao
hilo kupitia kwa Donald Ngoma aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kona wa Thaban
Kamusoko.
Mwanzoni mwa kipindi cha pili nusura Busungu aifungie Lipuli
bao lakini mpira wa kichwa aliopiga akiwa kwenye nafasi nzuri, ukapaa na kutoka
nje.
Dakika ya 76, Kamusoko alikosa bao la wazi, akiwa yeye na
kipa wa Lipuli, lakini kipa huyo Agathon Mkwano aliudaka mpira.
Katika mechi hiyo, Lipuli inayonolewa na mchezaji na kocha
wa zamani wa Simba, Selemani Matola, ilianza mchezo kwa kasi na kutawala katika
kipindi cha kwanza ambapo katika dakika ya 21 ilifanya shambulizi kupitia kwa
mshambuliaji wake Abdallah, lakini mpira wake wa kichwa haukulenga lango la
Yanga.
Dakika sita baadaye, Ngoma aliikosesha Yanga bao akiwa kwenye
nafasi nzuri lakini alipiga vibaya mpira wa kichwa na kutoka nje.
Yanga imecheza mechi hiyo ikitoka kufungwa kwa penalti 5-4
na mtani wake, Simba wiki iliyopita katika mechi ya Ngao ya Jamii kuashiria
kuanza kwa msimu mpya wa ligi.
No comments:
Post a Comment