Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Wednesday, July 26, 2017

MAHAKAMA YATUPA KESI YA TPBO, PST, TPBL DHIDI YA TPBC


MAHAKAMA kuu ya Tanzania imetupilia mbali kesi ya kampuni tatu zinazojihusisha na masuala ya ngumi kutokana na kutokidhi vigezo kwa mujibu wa sheria za nchi.
Kampuni hizo ni Puglist Syndicate of Tanzania (PST), Tanzania Professional Boxing Organization (TPBO) na Tanzania Professional Boxing Limited (TPBL) ambazo zilifungua kesi kupinga kusajiliwa kwa kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania TPBC) na kupewa majukumu ya kusimamia masuala yote ya ngumi za kulipwa nchini.
Kampuni hizo ziliungana kulitaka Baraza la michezo Tanzania (BMT) kutaja vigezo ilivyotumia kuipa usajili TPBC kusimamia ngumi za kulipwa kwakuwa hawana uwezo huo kisheria.
Kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama ya Temeke na Katibu Mkuu wa PST, Emmanuel Mlundwa lakini Mahakama hiyo ilishindwa kuisikiliza kutokana na kukosa nguvu kisheria.
Chaurembo Palasa (kushoto) akijadili jambo na Rais wa TPBO Yassin Abdallah ‘Ustadh’
Rais wa TPBC, Chaurembo Palasa amesema kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa na Jaji Kihiyo imetupiliwa mbali kwani BMT ipo kwa mujibu wa sheria za nchi hivyo ilikuwa sahihi kuipa usajili wa TPBC kusimamia masuala yote ya ngumi za kulipwa.
“Kesi iliyofunguliwa kwa ajili ya kuhoji uwezo wa BMT kuipa usajili TPBC kusimamia ngumi za kulipwa nchini imetupiliwa mbali kutokana na kukosa vigezo kwa mujibu wa sheria,” alisema Palasa.
Kutokana na ombi lao kukosa vigezo vya kisheria Mahakama Kuu imeamua kuliondoa shauli hilo na kuwataka walalamikaji kulipa gharama za kesi hiyo ambazo hazijawekwa wazi kwakuwa zinaandaliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kutokana na kushindwa kwa kesi hiyo TPBC itabaki kuwa Kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania na sasa inapaswa kuendelea na mchakato wa kuwa na vyama vya Mikoa.