Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Wednesday, July 19, 2017

DR. DAMAS NDUMBARO AACHIWA HURU NA KAMATI YA RUFAA Image result for NDUMBARO IMAGES
KAMATI ya nidhamu na rufaa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemwachia huru Wakili Dk. Damas Ndumbaro na aliyekuwa kocha msaidizi wa Geita Gold Mining Choki Abeid na kutupa rufaa nyingine tatu.
Akizungumza na wandishi wa habari jana Mwenyekiti wa kamati hiyo Rahimu Shaban alisema kamati yake ilikutana Jumapili kujadili warufani watano ambao ni Damas Ndumbaro, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tabora Yusuph Kitumbo na wenzake waliofungiwa maisha kujihusisha na soka.
“Tuliketi kusikiliza rufaa ya Damas Ndumbaro, Yusuph Kitumbo, Fechi Remtullah, Thomas Mwita na Choki Abeid na niwaeleze tu kwa kifupi kamati imemwachia huru Damas Ndumbaro baada ya kupitia vielelezo alivyowasilisha mbele ya kamati,”.
“Baada ya kamati kukaa na kupitia kwa kina maelezo ya Ndumbaro kamati ilijiridhisha kuwepo kwa mgongano wa kimaslahi kati yake na Mwenyekiti wa kamati hiyo Wakili Jerome Msemwa na pia hakupewa nafasi ya kusikilizwa japo alitoa udhuru kabla ya shauri kusilizwa,”
Ndumbaro aliwasilisha barua ya kujitoa kwenye kesi iliyokuwa inamhusu Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamal Malinzi hivyo kamati ilijiridhisha uwepo wa mgongano wa kimaslahi na pia hukumu iliyotolewa ilitolewa kwa wingi wa kura.
“Hukumu inasema imetolewa kwa wingi wa kura ambazo ni kura tatu za ndio dhidi ya moja ya hapana lakini haielezi kwenye akidi nani alikuwepo kwenye kikao hicho hivyo inatosha kueleza pasi na shaka kuwa akidi haikutimia,” alisema Shaban.
Aidha Shaban alisema kamati imeona ni busara kumwondolea kifungo hicho ambacho ameshatumikia kwa miaka miwili na miezi tisa toka afungiwe
Naye Choki Abeid aliyekuwa kocha msaidizi wa Geita Gold Mining amefunguliwa kutoka kifungo cha maisha kwasababu kosa lake haliendani na hukumu aliyopewa kwani alikuwa anatimiza majukumu yake.
“Kazi ya kocha ni kufundisha ili mchezaji acheze na soka ni mchezo wa kiungwana hivyo kocha kumsihi mchezaji kurudi uwanjani ili acheze ni moja ya majukumu yake,” alisema Shaban.
Kuhusu Yusuph Kitumbo, Fechi Remtullah na Thomas Mwita ambao walihikumiwa kifungo cha maisha kwa kujihusisha na kupanga matokeo ya mchezo wa Ligi daraja rufaa zao zimetupwa.
Awali Ndumbaro alifungiwa miaka saba na Kamati ya Nidhamu kutojihusisha na soka wakati akitetea klabu kuhusu maamuzi ya Kamati ya Utendaji ya TFF kukata fedha za udhamini wa klabu na mapato ya milangoni.
Ndumbaro alikuwa wakili wa klabu za ligi kuu hivyo ulikuwa wajibu wake kutetea wateja wake kukatwa asilimia tano ya fedha za udhamini na Sh. 500 ya kila tiketi inayokatwa na shabiki kuingia uwanjani.
Katika madai hayo Ndumbaro alidai kuwa Kanuni za Ligi zilizopitishwa kutumika kwa ajili msimu huu, hususan kuhusu makato ya fedha za milangoni si sahihi kwa vile zimerekebishwa na Kamati ya Mashindano ya TFF badala ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya shirikisho
Kamati hiyo ilimfungia Ndumbaro kwa kuzingatia Ibara ya 41(6) cha Kanuni za Ligi za TFF toleo la 2014 kujihusha na masuala ya soka ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 12.
 Na Ibara 41(16) cha Kanuni za Ligi za TFF toleo la 2014 kamati ilimfungia kutojihusisha na shughuli za soka ndani na nje ya nchi kwa miaka saba, hukumu iliyotolewa Oktoba 13, 2014.
Ndumbaro alikuwa mtu wa kwanza kufukuzwa uanachama wa TFF tangu Kamati mpya wa Utendaji ya shirikisho hilo chini ya Rais Jamal Malinzi iingie madarakani.