Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, May 21, 2017

CONTE ATAKUWA NA UENDELEVU CHELSEA? Image result for CONTE CHELSEA
ANTONIO Conte ni kocha mahiri na mwenye raha sana, miongoni mwa makocha wa klabu za Ligi Kuu ya England (EPL), kwa sababu amefanikiwa kutwaa ubingwa katika msimu wake wa kwanza Chelsea na England kwa ujumla.
Mtaliano huyu mwenye umri wa miaka 47, baada ya kupata mafanikio hayo, na pia kuingia kwenye fainali ya Kombe la FA itakayopigwa baadaye Uwanja wa Taifa wa England – Wembley, anatazamwa sasa na wadau mbalimbali, kuona iwapo maendeleo yenyewe yatakuwa endelevu.
Kuanzia wiki mbili zilizopita kumekuwapo tetesi kwamba huenda akaondoka, na kwamba Barcelona walikuwa wanatumia kila mbinu kumchukua, ili akazibe nafasi inayoachwa wazi na kocha wao, Luis Enrique aliyeamua kupumzika mwishoni mwa msimu huu.
Chelsea, wawe au wasiwe na Conte, wana mtihani Ulaya, kwani baada ya kuwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) wanarejea kwa kishindo msimu ujao, lakini pia mtihani mwingine ni kutetea ubingwa, jambo ambalo siku zote limekuwa gumu kwa timu nyingi, mfano wa karibu kabisa ukiwa ni wa Leicester waliotwaa pasipo kutarajiwa msimu uliopita na kulitema mapema msimu huu kwa kufungwa mfululizo hadi wakamfukuza kocha aliyewapa mafanikio hayo, Claudio Ranieri.
Baada ya kujihakikishia ubingwa, Conte alisema kwamba hiyo ilikuwa ndio mwanzo wake tu hapo Chelsea na kwamba mengi yalikuwa yanakuja, lakini mitaani watu wanasema akiisha kupata taji hilo anataka kwenda kwingine kukabiliana na changamoto mpya.
Wachezaji wa zamani wa Chelsea na waliokuwa na umaarufu kwenye maeneo tofauti, Ruud Gullit, Pat Nevin, Chris Sutton, Graeme le Saux na Mark Schwarzer wameitazama klabu yao ya zamani na wana maoni mbalimbali, ikiwa ni juu ya Conte na mengine jinsi klabu inavyoweza kujiimarisha ili kukabiliana na changamoto zilizo mbele yake.
Je, Conte atabaki? Taarifa kutoka nyumbani kwake, Italia, zinasema kwamba klabu ya Inter Milan, inayomwagiwa fedha nyingi na wafanyabiashara wa China, ipo tayari kumchukua Conte na kumpa mshahara wa pauni 250,000 kwa wiki – na hicho kinaweza kuwa kichochea cha yeye kuondoka Stamford Bridge iwapo Roman Abramovich hataangalia hilo.
Kuhusishwa kwake na kwenda Italia kunaangaliwa pia na ukweli kwamba mkewe na binti yao mwenye umri wa miaka tisa wamebaki huko baada ya Conte kuhamia jijini hapa mwaka jana. Ruud Gullit aliyecheza Chelsea na pia kuwa kocha kati ya 1995-98 ana maoni hapa:
“Nikizungumza kwa mtazamo wa kisoka, ni wazi kwamba atabaki. Changamoto yake ijayo ni kutwaa ubingwa wa UCL na anaweza kufanya hivyo na Chelsea. Ikiwa anahisi anayo timu inayoweza kushinda, kwa nini aondoke akaanze tena upya kabisa kwingineko?
“Hata hivyo ni jambo tofauti ikiwa ni uamuzi juu ya familia yake. Masuala yake binafsi ni muhimu pia. Familia yake hawapo London, na hii kidogo si kawaida kwa sababu nadhani hili ndilo jiji zuri zaidi ya yote duniani, sasa kwa nini hawaji? Hata hivyo, ingeeleweka ikiwa watu wanazifuata sana mila na dsturi zao. Na ikiwa wanafamilia wake wanataka kubaki Italia, basi ni uamuzi rahisi tu kwake kufanya.”
Pat Nevin aliyecheza mechi 250 akiwa na Chelsea kati ya 1983 na 1988 anasema kwamba baada ya kuzungumza na Conte kwa saa kadhaa wiki chache ilizopita, atashangaa iwapo ataondoka.
“Yaani hiyo itakuwa ofa isiyo ya kawaida kuweza kumwondosha Chelsea lakini kitu ambacho kwa kawaida huwafanya makocha wakaondoka kwenye nafasi kama yake ni pale wanapokuwa hawana uamuzi au wanaingiliwa kwenye mambo yao.
“Sidhani kwamba suala la fedha linaweza kumfanya aondoke na aliniambia kwamba anafurahia maisha ya London sasa. Kitu kingine cha kufikiria ni pale unaposimama Stamford Bridge na kusikia washabiki wakiimba 'Antonio, Antonio' ndipo unatambua kula mmoja anakuenzi. Kwenye hali kama hiyo ni ngumu kocha kuondoka,” anasema Nevin.
Chris Sutton aliyevunja rekodi ya Chelsea kwa kusajiliwa kwa pauni milioni 10 mwaka 1999 anasema kitu pekee anachoona kinaweza kumwondosha Conte Chelsea ni iwapo hatapewa fungu na kupata wachezaji anaowataka. Kwamba hadhani atatoa kipaumbele sana kwa UCL, maana atakuwa anataka kuchukua makombe yote ya nyumbani.
Conte alitwaa ubingwa wa Serie A – Ligi Kuu ya Italia mara tatu mfululizo kuanzia 2012, lakini hana rekodi nzuri kwenye UCL, kwani Juve walipigwa 4-0 kwa ujumla kwenye mechi za robo fainali msimu wa 2012/13 na msimu uliopita wakakwamia kwenye hatua ya makundi.
Graeme le Saux aliyecheza mechi zaidi ya 300 Chelsea kwa vipindi viwili tofauti vya kati ya 1987-1993 kisha 1997-2003 anasema endelevu wowote katika mafanikio unategemea na wafanyakazi, na kwamba iwapo Chelsea wataweza kubaki na wachezaji wenye kiwango, basi hawana tatizo.
"Eden Hazard na N'Golo Kante kila mmoja ana umri wa miaka 26 na huo ni umri mdogo, lakini kwa nguvu zao wana uwezo mkubwa wa kuwafanya Chelsea kuwa imara wakisonga mbele. Diego Costa amehusishwa na kwenda China lakini ni muhimu kwa Chelsea kubakisha kundi hili la wachezaji. Wakifanya hivyo, wataingia msimu ujao wakipewa nafasi kubwa ya kutetea ubingwa huu,” anasema Le Saux.
Mark Schwarzer aliyekuwa kwenye kikosi cha Chelsea 2014/15 anaona kwamba kuna uwezekano mkubwa kwa Chelsea kutwaa tena ubingwa wa EPL msimu ujao lakini pia ule wa UCL. Kuna wachezaji kadhaa kwenye kikosi hicho waliocheza mechi za UCL kwa mafanikio.