Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, April 16, 2017

KADHIA YA TIMU KUPOKWA POINTI SI KWA KLABU HATA TIMU ZA TAIFA.*Pointi zinazopokwa si lazima wapinzani wapewe

 USHINDI wa timu upo mara mbili – uwanjani na mezani; hii si kwa Tanzania tu bali hata huko duniani, ambapo ushindi wa uwanjani huweza kutenguliwa, mshindwa akapewa mshindi na mshindi akapewa unyonge.
Ndivyo ilitokea juzi kati hapa, ambapo Simba walipewa pointi tatu dhidi ya Kagera Sugar, kutokana na timu hii ya pili kuchezesha mchezaji ambaye hakuwa na sifa.
Kwenye mechi hiyo muhimu kwa Simba kuwania ubingwa, walifungwa na Kagera 2-1 na hivyo kuwapa wapinzani wao wa jadi – Yanga, mwanya wa kuwapiku kwa kutetea tena taji hilo. Hata hivyo, Simba walikwenda kukata rufaa, wakidai mchezaji Mohamed Fakhi alikuwa na kadi tatu za njano.
Kamati ya saa 72 ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) wamewapa Simba ushindi wa mabao 2-0 na pointi tatu hivyo kuwapaisha hadi pointi 61 katika nafasi yao ya kwanza, huku Yanga wakiwa nazo 56 na mchezo mkononi.
Simba jana ilicheza mechi nyingine ya ligi hiyo na Toto Africans Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, hivyo makala haya yameandaliwa kabla ya mchezo huo.
Visa vya jinsi hii vya ushindi wa mezani, ambao watu wengi huupinga na kusema bora mechi kurejewa, vimepata kujitokeza Tanzania, lakini pia kwenye sehemu nyingine katika ngazi ya klabu na pia ya timu za taifa.
Kwa Tanzania matukio kama haya yamepata kutokea, siku za mbele nitawaeleza katika makala nyingine, lakini kwa leo ngoja nizungumzie katika nchi zilizoendelea.
Matukio ya aina hii kwa nchi zilizoendelea kisoka ni machache, kwani kumbukumbu huwekwa vyema na wadau, ikiwa ni pamoja na kocha, mchezaji mwenyewe, na benchi la ufundi kwa ujumla.
Lakini pia chama cha soka huziweka na huweza kukumbushia klabu ili kuepuka fadhaa. Kuna sehemu nyingine watu huviziana tu, akicheza, hola! Ushindi wa mezani.
Kwa mfano kwneye Ligi Kuu za England, Hispania, Ufaransa, Italia, Ujerumani na kwingineko si rahisi kusikia mambo kama hayo.
Mchezaji kukosa sifa huwa ni kwa sababu mbalimbali, na si kuwa na kadi kadhaa za njano au moja nyekundu.
Mchezaji hukosa sifa ikiwa taratibu za usajili zilikiukwa, alishachezea timu mama (tuseme timu A) kwenye mashindano husika kabla ya kupelekwa kwa mkopo timu B. hata hivyo, imetokea katika EPL timu kuadhibiwa kwa kuchezesha wachezaji waliokosa sifa.
Kwa kawaida makocha ndio huingia kwenye aibu kwa kosa kama hilo. Hata hivyo, kupokwa pointi timu moja si lazima nyingine ipewe, na hii ilitokea 2010 baada ya mechi ambayo Brighton walifungwa 2-0 to Hartlepool United.
Kocha wa Brighton, Gus Poyet, alisonga mbele na kuandaa rufaa ili wapinzani wao wapokwe pointi na kuadhibiwa kwa sababu walichezesha mchezaji aliyekuwa na kadi, Gary Liddle.
Chama cha soka kweli kikafanya uchunguzi na kubaini mchezai huyo alikuwa amezuiwa kucheza, kikawapokonya Hartelepool pointi tatu na mabao mawili na kuwapiga faini ya pauni 3,500.
Hata hivyo, Poyet na Brighton waliachwa wamekasirika, kwa sababu hawakupewa pointi hizo, badala yake zilipelekwa kwa chama cha soka. Poyet alionesha hisia zake na kusema walikosea kabisa.
Mwaka 2014, timu ya Alfrteton Town walio Conference Premier ya England nao walipokonywa pointi tatu kwa kuchezesha mchezaji ambaye hakuwa na sifa wakapata ushindi wa 3-1 dhidi ya Kidderminster.
Golikipa Jon Worsnop, aliyekuwa amesajiliwa kwa mkopo wa dharyra kutoka FC United ya Manchester alicheza kwenye mechi hiyo, na kilichogomba ni kwamba hadi anacheza, bado kwenye mtandao usajili wake haukuwa umekamilika, hivyo watu wakaona na uamuzi kuchukuliwa.
Adhabu hiyo ni sawa na iliyokuwa imetolewa dhidi ya Oxford City na Harrogate Town, waliokiuka pia kanuni za ligi msimu huo.
Tukichambua zaidi tunawakuta jamaa wanaoitwa Rob Purdie na Jake Robinson wa Hereford United na Torquay Town wa England, ambapo katika mazingira yasiyo ya kawaida, timu zote zilichezesha wachezaji wasio na sifa.
Mechi ilimalizika kwa ushindi wa 3-1 kwa Hereford ambayo ilishuhudia kiungo Purdie na mshambuliaji Robinson wakicheza licha ya kwamba hawakuwa wamesajiliwa rasmi kwani dirisha la usajili la Januari lilitokea kufungwa kabla ya wao kuwa ndani, hivyo wakabaki nje.
Kila klabu ilimshitaki mwenzake kwa kukiuka kanuni za ligi, laiti wangekaa kimya, maana wote walilimwa faini ya pauni 17,500, kisha mshindi akapokwa pointi tatu na mshindwa pointi moja – faida kwa chama cha soka, kilichopata fedha na pointi zikarejeshwa kwenye shubaka.
 WACHEZAJI SITA WA FC SION
 Pengine kitu cha kutazama kwa mshangao ni kitendo cha timu ya Uswisi ya Fc Sion kuchezesha wachezaji sita wasio na sifa, nayo ilikuwa 2011. Adhabu yake ilikuwa kali sana, kwani walipokonywa pointi tatu kwa kila mchezaji batili, ikimaanisha walinyang’anywa pointi 36.
Yaani ukali wa adhabu ulimaanisha kwamba wamebaki na pointi hasi, maana hawakuwa nazo hata hizo walizonyang’anywa, na wakatupwa nje ya michuano ya Ulaya. Klabu hiyo wakati huo walikuwa chini ya marufuku ya usajili iliyowekwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Hata hivyo, kwa kichwa ngumu, walisonga mbele na kusajili wachezaji sita kisha wakawatumia kwenye mechi ya Ligi ya Europa dhidi ya Celtic wa Uskochi.
Awali Chama cha Soka (FA) cha Uswisi kilisita kuadhibu klabu hiyo had Fifa walipotishia kupiga marufuku timu ya taifa na klabu nyingine kushiriki michuano ya kimataifa.
Barani Afrika kuna kumbukumbu ya Guinea ya Ikweta kupokwa pointi tatu kutokana na kuchezesha mchezaji asiyekuwa na sifa kwenye mechi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Cape Verde.
Ajabu ni kwamba mchezaji mwenyewe anachezea klabu kubwa kiasi ya Hispania, Mallorca, naye ni Emolio Nsue Lopez, aliyecheza kwenye ushindi wa 4-3 Guinea ya Ikweta walioupata dhidi ya Cape Verde. Cape Verde walipewa ushindi na washindi wakapokwa.
‘Sinema’ haikuishia hapo, kwani Cape Verde nao waliishia kutupwa nje ya mashindano baada ya kuja kubainika kwamba nao walikuwa na mchezaji asiye na sifa ambaye alicheza. Walisikitika sana kwa sababu walishinda mechi mechi ya kuamua nani asonge mbele dhidi ya timu ngumu ya Tunisia.