Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, April 16, 2017

Man United vs Chelsea itakuwa raha leo




*Mourinho kujenga heshima baada ya kupigwa 4-0?
*Conte anataka kuonesha hakubahatisha hapo awali

 LEO kuna mambo makubwa, wakati Wakristo wakiadhimisha ibada ya Pasaka na sherehe zake, kwenye soka kuna mechi kubwa baina ya vinara wa ligi, Chelsea wanaokaribishwa na Manchester United.
Chelsea wamefunga safari kwa ajili ya mechi hii wakiwa wanajiamini zaidi, lakini pia wakifurahia uendelevu wa kuwapo kwao kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu ya England (EPL) kwa idadi kubwa ya pointi, United wakiwa nafasi ya tano.
Wakati Chelsea wamejikusanyia pointi 75 katika mechi 31, United ambao wamekithiri kwa sare wanazo pointi 54. Chelsea wanafurahi kuwakabilia Man U wikiendi hii, kwani wametulia kwa siku nane bila kucheza mechi.
Tofauti kabisa, wapinzani wao, Manchester United wanaingia uwanjani baada ya safari ya Ubelgiji walikotoka kucheza na Anderlecht katika mechi za Ligi ya Europa Alhamisi iliyopita dhidi ya Anderlecht ya hukomchezo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1jambo ambalo hapana shaka limewaongezea uchovu.
Antonio Conte anatambia mwenendo wa kuridisha wa Chelsea hadi sasa katika msimu wake wa kwanza hapa England wakati Jose Mourinho bado anaendelea kukisuka kikosi chake, kwa kuangalia nani akae wapi.
Old Trafford inatapika leo kwa ajili ya watu kushuhudia mechi hii kubwa, wakiwa ni washabiki wa United wenyeji lakini pia wale wa Chelsea walio Manchester na wengi zaidi wanaosafiri kuwaunga mkono vijana wao.
Timu mbili hizi zinapokutana huwa kuna mengi ya kuvutia, iwe ni mwanzoni mwa msimu au hata mwishoni kama sasa, bila kujali ni timu ipi bingwa, iliyo mbele ya mwenzake kwenye msimamo wa ligi au wanapishana vipi.
Huwa ni wakati wa kulinda heshima, kila mmoja akitaka mwingine amheshimu. Ni sahihi kusema kwamba mechi baina ya fahali hawa wawili ni moja kati ya zinazokuwa moto zaidi na kwa kawaida washabiki huwasha fashifashi.
Hata hivyo, haikuwa hivi tangu zamani, kwa sababu uhasama baina ya klabu mbili hizi si wa jadi bali umekuja katika zama hizi. Uhasama wa jadi ni baina ya Manchester United na Liverpool na huo ni kitaifa, wakati Chelsea mahasimu wao ni Arsenal, na hao ni wa jijini London.
Uhasama kwenye soka hapa nchini, pamoja na mambo mengine, umetokana na mambo kadhaa, yakiwamo eneo la jiografia klabu zinapotoka au ushindani uliozidi sana kwa ajili ya kuwania heshima baina ya klabu mbili husika.
Wanaocheza leo wapo mbalimbali sana, wanatenganishwa na umbali wa maili 170, njiani humo, au kwenye mizingo, kukiwa na klabu nyingine nyingi tu, zikitenganisha fahali hawa wawili. Ni kwa msingi huo, nasema kwamba huu ni ushindani wa kuwania heshima na si ule wa eneo la kijiografia.
Klabu zote mbili wamepata kufurahia mafanikio kabla ya zama hizi, kwenye miaka ya ’50 na mwishoni mwa ’60, wakati United ya zama za Matt Busby – lakini zama za sasa hazingeweza kuwekewa uendelevu mrefu wa kutosha kwazo kushinda ilhali uhasimu kwa asili haukupata kuundwa.
Baada ya tasa ya miaka 26, Manchester United, chini ya Alex Ferguson walitwaa ubingwa wao kwa mara ya kwanza 1993 na tangu hapo ukaanza ujenzi wa kile kilichoitwa moja ya ngome imara za soka katika historia ya England.
United walipata kuja kuingia kwenye uhasimu fulani ulioburudisha sana dhidi ya Newcastle, lakini ulichukua muda mfupi kabla ya Arsenal kuwapandia na kutaka kuwapokonya chakula kwenye sahani na kuwa wapinzani wakubwa na tishio ka Fergie mwishoni mwa miaka ya ’90 na mapema miaka ya 2000.
Baadhi ya vita ambazo klabu mbili hizi zimepigana zitabaki kwenye kumbukumbu ya muda mrefu. Kuwasili kwa bilionea wa Urusi, Roman Abramovic Stamford Bridge na kuonwa kama mifuko yake haioni mwisho 2003 kulionesha mwanzo wa ushindani mkubwa baina ya klabu hizi.
Kwa nini? Ieleweke kwamba United ni moja ya klabu kubwa hapa England lakini hata Ulaya, hivyo walikuwa wakitamba sana England, sasa kuibuka kwa bilionea ambaye anamwaga fedha, anasajili wachezaji wakubwa, hachukui gawio mwaka wa fedha ukikamilika kunawatisha wapinzani.
Manchester wakaona kwamba mambo si rahisi tena, hali si lele mama bali lazima kujituma hasa ndani na nje ya uwanja. Abramovich akamleta Jose Mourinho London, na baada ya kuwa bila ubingwa tangu 1955, Chelsea (mpya sasa) wakatwaa ubingwa wa England.
Mourinho ni wa kushukuriwa kwa jinsi alivyowajenga Chelsea wakawa walivyo kabla ya kuondoka, akarejea mara ya pili, akaboronga na kufukuzwa kisha akajiunga upande wa pili – Manchester United, na leo wanacheza, ikiwa ni mechi yake ya pili akiwa huko.
Ile ya awali msimu huu, ilifayika Oktoba 23, siku ya Jumapili kama leo, na Mourinho aliondoka huko kwa aibu kubwa, kwani Conte hakumwonea huruma, akiwaacha vijana wake kuwasasambua Mashetani Wekundu 4-0.
 Mreno huyu (Mourinho) alitumia vyema fedha za bosi wake kutwaa ubingwa mara mbili, Kombe la FA na makombe mawili ya Ligi katika kipindi cha miaka mitatu iliyokuwa kama ya upepo wa kinyamkera jijini London.
Wakati klabu mbili hizo zilikuwa zikipigania heshima dimbani, nje ya uwanja Fergie alikuwa akifurahia vijembe vyake dhidi ya makocha wengine, na ilifika mahali Mourinho akadai kwamba Fergie hakuwa na heshima isipokuwa kwake mwenyewe.
Kupigana kwao vijembe na kutunishiana misuli kuliambukizwa kwa wachezaji wao pia, ambapo kwenye mechi kulikuwa na undava pia, lakini kila upande ukitaka uibuke na ushindi.
Mourinho alipoondoka kwenda kuwafundisha Real Madrid, Ferguson alisema ‘Ligi Kuu imempoteza kijana mwenye bunduki aliyekuja mjini akitaka kupambana na mzee mlinda Amani.”
Wawili hao walikuja kuonekana wakijenga urafiki, ikadhaniwa Mourinho alikuwa akivizia kupewa kazi baada ya Fergie kustaafu, lakini hakupewa, badala yake akapewa Mskochi mwenza na Fergie, David Moyes, aliyefukuzwa miezi 10 tu baadaye.
Hata hivyo, aliipata kazi hiyo baada ya kocha mwingine, Louis van Gaal kushindwa misimu yake miwili na kutimuliwa, wakati Mourinho naye akiwa hana kibarua baada ya kufukuzwa Chelsea alikofanya vibaya kiasi cha kuielekeza timu kwenye kushuka daraja.
Leo sasa katika mechi ya pili dhidi ya timu yake ya zamani aliyosema aliipenda sana, Mourinho anataka kuwaonesha kwamba yeye ni zaidi, lakini pia alipe kisasi cha kufungwa 4-0 mechi ya kwanza, jambo ambalo linaonekana zito kiasi, lakini kwenye soka wanasema mpira unadunda, hivyo lolote linaweza kutokea.

Kwenye bodi za wakurugenzi kumebadilika, ambapo Peter Kenyon yeye aliondoka United kwenda Chelsea, akisema kwamba waajiri wake wapya wangekuwa klabu kubwa zaidi duniani ikifika 2016; bado hawajawa, mwaka mmoja baadaye.
Fergie alichukia kuondoka kwa Kenyon, akisema iweje aende kwenye klabu isiyokuwa na historia ya kabla.

Washabiki wa United wanasema kwamba kwao, mahasimu wanaotangulia ni Liverpool, Manchester City, Leeds United kisha ndio matajiri hao wa London. Chelsea wao wanasema wanaanza na Arsenal kisha Tottenham Hotspur.
Historia ya karibuni ya timu hizi mbili inaonesha kuwa wachovu kiasi, kushindwa kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), lakini Chelsea wanaonekana kurudi huko mwaka huu, wakati United wanatakiwa kukaza msuli ili kuwapiga kumbo Man City na Arsenal washike nafasi ya nne.


No comments:

Post a Comment