LICHA ya
kufanya vyema kwenye msimu ambao uliwapatia Leicester ubingwa wa England, ni
wachache waliomzungumzia Onyinye Wilfred Ndidi.
Hii, kwa
kiasi kikubwa, ni sababu ya kuwapo kwa kiungo mwingine, N’Golo Kante, aliyekuwa
injini ya timu hiyo kabla ya kununuliwa na matajiri wa London, Chelsea.
Kundoka kwa
Kante kumefungua mlango wa dhahabu kwa Ndidi, ambaye sasa anawika King Power
Stadium, tena akionesha uwezo wa kumzidi Kante.
Ligi Kuu ya
England (EPL) ina vipaji muhimu na adimu, na ni kama hivi vinavyokua sasa,
baada ya kusajiliwa hapo kutoka Genk kwa pauni milioni 15 Januari.
Huyu ni
mchezaji wa kimataifa wa Nigeria ambaye kwa bahati mbaya ya Leicester, tayari
ameanza kuhusishwa na uhamisho kwenda ama Manchester United au Arsenal,
kutokana na mfuatano wa mechi alizoonesha kiwango cha hali ya juu.
Ukimwangalia
vizuri utaona kwamba kuna maeneo hata anamzidi Kante, japokuwa wengi ukiwauliza
hilo hawataki kusikia lolote juu ya kusema Kante yupo chini – ni mtu
anayependwa sana, lakini huyu naye watampenda tu.
Kama Kante,
Ndidi ana stamina ya aina yake na inayotakiwa EPL, huku akiwa hana woga
kuingiza mwili wake mahali kwa ajili ya kutaka kuuchukua mpira kwa adui –
hahofii kuumia, na haumii hovyo.
Alipofanya
makabiliano 10 katika dakika 65 tu dhidi ya Liverpool, alifupisha mambo mengi
yaliyomsababisha bosi Craig Shakespeare kumsajili baada ya kufukuzwa kazi kocha
aliyewapa ubingwa, Claudio Ranieri. Takwimu
hizo zinakaribia zile za Kante ‘mharibifu wa ukweli’.
Uwezo wake
wa kutoa pasi za uhakika ni mkubwa na jicho kwa mpira, hasa anapotoka mbali, na
hili ndilo limekuja kubadili mwelekeo wa Leicester kuanzia alikoachia Ranieri,
anayeziba ombwe la Kante ni Ndidi.
Mwanasoka
huyu anasema kwamba amekulia kwenye mazingira magumu ya kijeshi jijini Lagos na
anaamini hali hiyo ndiyo imempaisha hadi kufikia kuja kumshika mweusi
mwenzake, Kante, japo huyu wa pili anatoka Ufaransa.
Anasema
akiwa maeneo hayo ya kambi za kijeshi, alikuwa na nguvu na uwezo wa kukimbia,
ambapo baba yake aliyekuwa mwanajeshi hakutaka awe mwanasoka, hivyo alifurahi
sana alipopelekwa kwenye operesheni za kulinda amani.
Hakutarajia
angekuwa katika kikosi cha kwanza cha timu inayocheza EPL hata kidogo, kwa
sababu mipango yake haikwenda vyema awali. Ilikuwa Julai 2015, miezi sita ya
mwanzo ya Ndidi huko Genk akiwa kana kwamba hayupo; ikawa ngumu sana chini ya
kocha Alex Mcleish.
Kuwasili kwa
kocha mpya, Peter Maes kulibadili mazingira na fursa za Ndidi, akaanza kufanya
vyema, hasa kwenye mechi ya kwanza dhidi ya OH Leuven na timu nyingine kubwa
kama mabingwa Gent.
Anasema
kulikuwa na shinikizo kubwa juu yake, akiwa na umri wa miaka 18, pasipo na
uzoefu wowote mkubwa.
“Nilikuwa na
wasiwasi mkubwa na sikuweza hata kutoa pasi vizuri, nilipelekwa kwenye nafasi
mpya na kocha hakuwa aina ya wale ambao hutulia, anabwatukia kila mchezaji na
baada ya nusu ya kwanza akanitoa uwanjani. Mapumziko tu!
Anasema
baada ya hapo alikaa benchi mechi kadhaa, lakini akajifua sana na aliprudi tu,
nyota ikawa imewaka tena na baada ya kuhamia Leicester, ni tegemeo kubwa na
tishio kwa wachezaji wa timu pinzani.
Alianza
kuonesha vitu adimu, na sasa Leicester wanasema hawajutii kuondoka kwa Kante,
japokuwa tena wana shinikizo juu yao, kutokana na klabu kubwa kumtolea macho
ili wamchukue.
Ana sifa ya
kufunga mabao machache, lakini akifanya hivyo ni kwa staili ya aina yake, na
alifanya hivyo kwenye mechi ya Kombe la FA dhidi ya Derby County, akaonesha
tena dhidi ya Stoke kwa mpira wa mbali, aina ya mchezo inayoonesha kwenda
kinyume na umri wake mdogo.
Imewachukua
mabingwa watetezi hawa miezi sita kupata mtu wa kuvaa viatu vya Kante, laiti
Ranieri angemuona Kante alipoondoka, basi si ajabu wangetetea taji lao, maana
sasa wako vyema, lakini muda umewatupa mkono, kwani wameachwa mbali sana na
timu nyingine.
Ndidi
ana umri wa miaka sita pungufu ya Kante na amenunuliwa kwa pauni milioni 17,
akiwafaa sana, akicheza kwenye timu iliyokuwa ikipambana kuepuka kushuka daraja
hadi wiki chache zilizopita.
Anakataa
kujifananisha na Kante, au kuzungumzia juu ya kufananishwa huko akisema:“Naweza
kujiona mwenyewe kama mimi tu, iwe watu wanasema kwamba nacheza kama Kante au
ni mzuri kuliko yeye au yeye mzuri kuliko mie siwasikilizi, ninachotaka ni
kucheza tu na kuzidi kuboresha kiwango changu, kufanya kazi kwa bidii ndilo
lengo langu kwa sasa.
“Sie
tunafanya yale mambo ya msingi, na mie hupenda kuwa na mawazo, imani na nguvu
ya kushinda siku zote, nikifanya kazi na wenzangu kitimu kuliko kuwaza na
kusimulia nacheza kama nani.”
Baba yake
alikuwa akienda kulinda amani kwenye nchi kama Sudan pamoja na maeneo
yaliyochafuka ya kaskazini mwa Nigeria mara kwa mara, na Ndidi alifurahi babaye
alipoondoka.
“Nilikuwa
nafurahi sana alipoondoka kwa sababu hakutaka nicheze mpira, bali nitie juhudi
shuleni. Kila akiondoka nilijisemea sasa ni wakati wangu wa kucheza hasa,”
anasema.
Zilikuwapo
timu rasmi zilizopangwa za wajeshi, kuanzia chini ya umri wa miaka 10 hadi za
wakubwa, hivyo akiwa tineja alionwa na Nduka
Ugbade,
aliyekuwa nahodha wa Nigeria kwenye mechi za Shirikisho la Soka la Kimataifa
(Fifa) U-16.
Alikuwa
miongoni mwa waliokuwa mabingwa 1985 na sasa alikuwa kwenye kambi za kijeshi
akifundisha soka. “Nadhani nilichokifanya naye ilimaanisha kwamba nilikuwa na
nguvu kuliko watu walivyotarajia niwe nazo nilipokwenda kukabiliana nao uwanjani,”
anasema.
Anakumbukia
aina ya mateso aliyopata, ikawa kama adhabu kwake kwenye jeshi, kumbe ilikuwa
ni kipaji kinafinyangwa na Ugbade.
Alipata
nafasi Akademia ya Nath Boys, moja ya shule za soka zinazothaminiwa zaidi
jijini Lagos na ni hapo jitihada za Ugbade za vipindi vya mazoezi zilipozaa
matunda.
Ndidi akiwa
na umri wa miaka 16, Nath Boys waliingia kwenye mashindano yaliyoshirikisha
timu 40 na ilikuwa akademia dhidi ya timu za wakubwa hata kutoka Ligi Kuu ya
Nigeria.
Kati ya
maskauti waliokuwa wakifuatilia mashindano hayo ni Roland Janssen, enzi hizo
akiwa Genk na sasa anafanya na Manchester United.
Anasema
ushawishi wake kwenye soka na nafasi hiyo ni kumtazama Nahodha wa Chelsea, John
Terry, akatwaliwa na Genk, akaingia kwenye timu ya taifa ya vijana na sasa yupo
na ya wakubwa, huku klabu kubwa kabisa Uingereza zikimtazama.
No comments:
Post a Comment