Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Thursday, April 27, 2017

FRANK KOMBA; WAKILI ANAYEKWENDA KUCHEZESHA AFCON U-17 GABON

Mwamuzi kuchezesha mashindano makubwa siyo bahati ni uwezo wake.

Na Rahel Pallangyo
“KATIKA soka nakerwa na tabia ya kuhusishwa na ushabiki wa Simba na Yanga hasa kwa sisi waamuzi wa soka,” hayo ni maneno ya awali ya Frank Komba ambaye ni mwamuzi msaidizi wa soka mwenye beji ya FIFA.
Komba pamoja na hiyo changamoto ya waamuzi  kuhusishwa na ushabiki kwenye soka hajakata tamaa ya kuendelea kujifunza zaidi kuhusu sheria za soka kwa kuangalia jinsi waamuzi wengine wanavyochezesha au kwa kukaa darasani na kudurusu sheria 17.
“Mimi pamoja na kubanwa na kazi najitahidi kila siku kukutana na wenzangu kwenye Uwanja wa Karume na kufanya mazoezi na kudurusu sheria za soka kwani kuna mambo yanafanyiwa mabadiliko kila mwaka,” alisema Komba ambaye ni mkufunzi wa sheria kwenye Chuo cha maofisa wa polisi Kurasini.
Bidii, kujituma na kufanya vizuri kumemfanya Frank Komba awe miongoni mwa waamuzi ambao watachezesha faibnali za vijana za Afrika zitakazofanyika nchini Gabon kuanzia Mei 14 na Tanzania ikiwakilishwa Serengeti boys.
Komba yupo kwenye orodha ya waamuzi wasaidizi (Assistant Referees) na ni mwamuzi pekee kutoka Tanzania aliyepata fursa hii adhimu kati ya waamuzi wasaidizi 15 na waamuzi wa kati 14 Afrika nzima.
 Komba anaungana na waamuzi wengine wawili kutoka ukanda wa Afrika Mashariki ambao ni Pacifique Ndabihawenimana wa Burundi na Davies Ogenche Omweno wa Kenya ambao ni mwamuzi wa kati.
Komba ambaye alipata beji ya FIFA 2015 anasema kuchaguliwa kuchezesha fainali hizi si kwa sababu Tanzania ina timu kwenye mashindano hayo bali inatokana na uwezo wake kwani kuna waamuzi kadhaa ambao wamechezesha fainali mbalimbali lakini hakuna timu kutokam kwenye nchi zao.
Marehemu Hafidh Ally alichezesha fainali za vijana za dunia (U-16) 1989 zilizofanyika  nchini Scotland akiwa na waamuzi wengine wawili kutoka Afrika, na Jonesia Rukyaa mwaka jana amechezesha fainali za Afrika kwa wanawake lakini Tanzania haikuwa na mwakilishi bali ubora wao ndio uliowafanya wachaguliwe.
Wapo pia Fernand Chacha ambaye alichezesha U-15 zilizofanyika Botswana 2015 na All African Games 2016 zilizofanyika Congo Brazaville,   Omar Abdulkadir, Saada Tibabimale nao wamechezesha mashindano makubwa Afrika, ukiacha hawa wa Tanzania, mwamuzi msaidizi wa Burundi, Jean Claudie Birumushahu  alichezesha fainali za Afrika dhidi ya Misri na Cameroon  zilizomalizika Januari mwaka huu.
KUHUSU AFCON U-17 GABON
Komba anasema anakwenda kuwa balozi mzuri wa waamuzi wa Tanzania kwenye fainali za Gabon huku akiwataka kumwombea ili afaulu mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness) ambao watafanya Mei 9 nchini Gabon.
“Kila mashindano lazima ifanyike Physical fitness kabla ya kuanza mashindano na endapo mwamuzi atafeli basi hatopangwa kuchezesha, nimejiandaa na muombba Mungu anisaidie ili nikafanye vizuri maana lolote linaweza lakini ukimtanguliza Mungu kwake yeye kila gumu hilifanya jepesi,” alisema Komba baba wa mtoto mmoja wa kike, Britney
Pia Komba anasema ataonesha kuwa waamuzi na soka la Tanzania liko mbali kwa kutafsiri vema sheria 17 za soka.
KUHUSU WAAMUZI
Komba anawaasa waamuzi kupendana, kushirikiana kwa kila kitu wakiwa mchezoni, kabla ya mchezo na baada ya mchezo na kwenye mambo ya yanayohusu maisha yao ya kila siku.
“Waamuzi tuna ile tabia ya kupenda kumsema mwenzeko idha pale anapokuwa anauliza maswali kwa kumuita kiherehere jambo ambalo siyo nzuri tunatakiwa tupendane kwani sisi ni familia moja maana wanaposema waamuzi nje tunasemwa wote,” alisema Komba.
KUHUSU ELIMU
Komba mtoto wa Profesa Francis Magingo  wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani amefuata nyayo za baba yake kwani ni mhitimu wa Shahada ya Sheria  (LLB) aliyopata kwenye Chuo cha Ruaha, Tawi la Chuo cha Saut kuanzia mwaka 2007- 2011 na baadae kujiunga na Law School of Tanzania 2011-2012 na kutunukiwa Post Graduate, Diploma in Illegal Practice.
Mwaka 2012-2013 alijiunga na Chuo cha Polisi Moshi ambapo alitunukiwa Cheti cha awali cha polisi na kuajiriwa kwenye Chuo cha Maofisa wa polisi kama mkufunzi wa sheria ambapo anafanya kazi hadi sasa.
Mwaka 2016 alitunukiwa kuwa wakili baada ya kuonekana kuwa na mwenendo mzuri katika kazi yake ya sheria.
Komba ambaye alizaliwa 1984 na mama Christina Francis Magingo  alisoma Shule ya Sekondari ya Loyola  kuanzia kidato cha kwanza 2000  hadi cha sita ambapo alihitimu 2007 katika mchepuo wa HGL.
Alisoma shule ya msingi Mlimani kutoka darasa la kwanza hadi la saba 1993-1999.
KUHUSU FAMILIA
Komba mwenye miaka 35 amemuoa Voileth David na wamejaliwa mtoto mmoja wa kike, Britney.
Pia Komba anawashukuru wazazi wake Profesa Francis Magingo na Christina Francis Magingo  kwa malezi bora waliyompatia , elimu na hatimaye sasa amekuwa baba wa familia kwani hana cha kuwalipa zaidi ya kuwaombea maisha marefu.
Kipekee anamshkuru mke wake Vaileth kwa upendo ambao haujawahi kupungua kuanzia uchumba hadi sasa kwani anajua kuna wakati anakosa uhuru wa kukaa naye karibu kwa kutambua majukumu yanayomkabili.
“Wote tunafanya kazi lakini mimi majukumu yangu yanazidi kwa sababu kwenye uamuzi nahitajika kusafiri na kufanya mazoezi sasa inawezekana muda mwingine amepanga kuwa karibu na mimi hasa siku za mwisho wa wiki au jioni lakini ananikosa, nashukuru anaelewa majukumu yangu,” alisema Komba
ALIJIUNGA LINI NA UAMUZI?
Komba anasema kipindi anasoma Shahada ya sheria kwenye Chuo cha Ruaha Iringa akiwa katika matembezi mwaka 2008 alikuta tangazo la mafunzo ya awali katika duka la vifaa vya michezo.
Baada ya kulisoma alitafuta zilipo ofisi cha Chama cha Soka Mkoa wa Iringa na kujiandikisha, akakubaliwa, akaingia darasani chini ya mkufunzi Mchungaji Lugenge na Ramadhan Mahano.
“Ilibidi nijiunge na urefa kwa sababu nilikuwa napenda soka lakini kukosa muda wa kufanya mazoezi kila mara na uhaba wa viwanja nililazimika kuingia upande wa pili ili niwe nachezesha,” alisema Komba
Komba anasema darasa lao walikuwa kumi na yeye pamoja na Janeth Balama wamebahatika kuwa na beji za FIFA huku wengine wakichezesha soka katika ligi mbalimbali.
Fainali za AFCON U-17 zinatarajiwa kuanza Mei 14 -28 na Tanzania itawakilishwa na timu ya taifa ya vijana ya Tanzania ‘Serengeti Boys’ ambayo ipo kwenye kundi B na timu za Ethiopia, Niger na Angola, wakati Kundi A lina timu za wenyeji, Gabon, Guinea, Cameroon na Ghana.