Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Saturday, October 1, 2016

SERENGETI BOYS KUCHEKA AU KULIA KESHO?


TIMU ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kesho  itakuwa mgeni wa Congo Brazzaville katika mchezo wa mwisho wa kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo.

Serengeti Boys itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu  ya kushinda mchezo wa nyumbani dhidi ya timu hiyo ya Congo mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hivyo katika mechi ya leo, Serengeti inahitaji kulinda mabao hayo huku ikiongeza mengine kwani timu itakayoshinda itafuzu fainali hizo zitakazofanyika Madagascar mwakani.

Katika kuhakikisha inafanya vizuri kwenye mchezo huo, Serengeti iliweka kambi ya siku sita Kigali, Rwanda kufanya maandalizi ya utulivu na kuwajenga wachezaji kisaikolojia kwa ajili ya mchezo huo.

Kocha wa Serengeti Boys, Bakari Shime akizungumzia mchezo huo alisema hautakuwa rahisi kwani Congo ni timu nzuri yenye vijana wazoefu na mashindano hayo.

“Mchezo utakuwa  mgumu lakini silaha zangu zipo tayari kwa mchezo, naamini tuna uwezo wa kushinda, kama wao walipata mabao kwetu, hata sisi tukipambana tutapata,”alisema.

Awali, Serengeti Boys ilivuka raundi hii ya mwisho baada ya kuzitoa Shelisheli kwa jumla ya mabao 9-0, ikishinda mchezo wa nyumbani 3-0 na ugenini 6-0.

Pia, iliitoa Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 3-1, ikitoka sare ya bao 1-1 ugenini na kushinda nyumbani mabao 2-0.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye aliahidi timu hiyo Sh milioni moja kwa kila bao litakalofungwa kama motisha ya kuonesha juhudi na kuvuka hatua nyingine.

Ikifuzu, itakuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufika hatua hiyo. Iliwahi kufanya hivyo kwa timu ya wakubwa Taifa Stars mwaka 1980 michuano ya Kombe la Mataifa Afrika ilipofanyika Lagos, Nigeria.

Serengeti Boys iliwahi kufuzu michuano iliyofanyika mwaka 2005 Gambia, lakini iliondolewa baada ya kubainika kumtumia mchezaji aliyezidi umri.

Mwisho.