YANGA
imerejesha furaha kwa mashabiki wake baada ya leo kushinda mabao 3-0 dhidi ya
Majimaji katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es
Salaam.
Mabingwa
hao watetezi wa ligi hiyo wamepata ushindi baada ya kutoka sare ya bila kufungana katika
mechi dhidi ya Ndanda iliyochezwa Mtwara, Jumatano ya wiki hii.
Yanga
ilipata bao la kuongoza katika dakika ya 20, likifungwa na Deus Kaseke
aliyeuwahi mpira wa penalti iliyopigwa na Simon Msuva.
Awali,
mwamuzi wa mechi hiyo Emmanuel Mwandebwa wa Arusha alitoa penalti kwa Yanga
baada ya mchezaji wa Majimaji kushika mpira eneo la hatari na ndipo Msuva
alipopiga penalti mara ya kwanza, lakini mwamuzi alimtaka kurudia tena akidai
alikosea, akaipiga mara ya pili ikaamuliwa kurudia tena, akapiga mara ya tatu
mpira ukagonga mwamba na ndipo Kaseke alipouwahi na kuujaza wavuni.
Kipindi
cha kwanza kiliisha kwa Yanga kuongoza kwa bao 1-0. Katika kipindi hicho, Yanga
walitengeneza nafasi nyingi lakini walishindwa kuzitumia huku Majimaji
wakicheza kwa kuzuia zaidi.
Amisi
Tambwe aliifungia Yanga bao la pili dakika ya 81 kwa kichwa, ikiwa ni baada ya
kufunga katika dakika ya 74 na mwamuzi kulikataa akidai mfungaji aliotea.
Dakika tano baadaye, Tambwe aliongeza bao la tatu kwa pasi ya Juma Mahadhi.
Kutoka
kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya, Azam jana iliendelea kuzoa pointi kwenye uwanja
huo baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-1.
Kwenye
uwanja wa Nangwanda Sijaona, Ndanda ilitoka sare ya bila kufungana na Kagera
Sugar. Huku kwenye uwanja wa Mwadui Shinyanga, Mwadui imetoka sare ya mabao 2-2
na Stand United.
Katika
uwanja wa Mabatini Mlandizi, Ruvu Shooting iliitambia JKT Ruvu kwa kuifunga bao
1-0.
Ligi
hiyo inaendelea tena leo kwenye uwanja wa Uhuru ambapo Simba itaikaribisha
Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani.
Mechi
hiyo inatarajiwa kuwa kali na ya vuta nikuvute kutokana na timu hizo kutambiana
kwa zamu kila zinapokutana.
Timu
hizo zinakutana zikiwa na makocha wapya Joseph Omog wa Simba na Salum Mayanga
wa Mtibwa na wote wakionesha kuwa wanalitaka taji kulingana na ubora wa vikosi
vyao.
Mtibwa
Sugar inapokutana na Simba au Yanga ni wazi kuwa hucheza kwa kukamia, lakini
mwisho wa siku mmojawapo huibuka na ushindi.
Msimu
uliopita timu hizi zilikutana raundi ya kwanza Januari 16, mwaka huu Simba
ikaibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa,
pia ilipokutana katika raundi ya pili Mei 15, mwaka huu bado Simba ilishinda
bao 1-0.
No comments:
Post a Comment