SIMBA leo imetoa vitisho kwa wapinzani wao wa jadi Yanga baada ya kuifunga
Majimaji ya Songea kwa mabao 4-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Yanga na Simba zinapambana Jumamosi ijayo kwenye Uwanja huo wa Taifa
katika mchezo wa ligi hiyo unaotarajia kuwa mkali na kuvutia kufuatia ubora wa
timu hizo.
Msimu uliopita, Simba alifungwa na Yanga mabao 2-0 katika mechi zote
mbili na hivyo kusababisha unyonge kwa wapenzi wake dhidi ya wapinzani wao hao.
Katika mchezo wa jana, Simba waliandika bao la kwanza katika dakika ya
nne lililowekwa kimiani na Jamani Mnyate.
Mashambulizi ya Simba yaliongozwa na Mohamed Hussein Shabalala na hadi
mapumziko wenyeji walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Majimaji walipiga shuti la kwanza langoni mwa Simba katika dakika ya 28
lakini halikuzaa matunda.
Simba waliandika bao la pili katika dakika ya 62 kwa penalti
iliyofungwa na Kichuya baada ya Shabalala akichanja mbuga kuelekea langoni na
kumpiga kanzu beki wa Majimaji aliyeunawa mpira na kuwa penalti.
Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi wa Tabora Ludovic Charles.
Jamal Mnyate aliiandikia Simba bao la nne katika dakika ya 75 kwa shuti
kali lililomshinda kipa wa Majimaji Amani Simba na mpira kujaa wavuni.
Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 16 na kuzidi kujichimbia
kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha jumla ya timu 16.
Katika mchezo mwingine, Azam FC jana walikiona cha moto baada ya
kuchapwa bao 2-1 na Ndanda FC katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa
Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Mtibwa walitoka sare ya kufunga 1-1 na Mbao katika mchezo uliofanyika
kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani.
Wakati huohuo, Simba kesho Jumatatu inakwenda Zanzibar kuweka kambi kwa
ajili ya kukabiliana na Yanga katika mchezo utakaofanyika Jumamosi.
No comments:
Post a Comment