MATOKEO ya sare ya bila kufungana yameifanya Simba ya msimu
huu isiwe na tofauti na ile ya msimu uliopita ambapo ilikuwa ikipata matokeo
yake kama homa ya vipindi.
Simba ilianza ligi kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ndanda
katika mechi ya kwanza lakini jana ilishindwa kuendeleza wimbi hilo la ushindi
baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na JKT Ruvu katika mechi
iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Huku mashabiki wake wakitarajia kupata ushindi jana,
walijikuta wakitoka uwanjani mapema na wengine kutoka vichwa chini baada ya
matokeo hayo.
Katika mechi ya leo Simba ilitawala karibu katika kila
idara kuanzia dakika ya kwanza ya mchezo lakini wachezaji wake walikosa mabao
mara kadhaa kila walipolifikia lango la wapinzani wao.
Ni katika kipindi cha kwanza mchezaji Shizza Kichuya
alipoteza nafasi kadhaa za kufunga hasa ile ya dakika ya 36 ambayo aliwalamba
chenga mabeki wa Ruvu lakini alishindwa kumalizia na kuporwa mpira huo.
Mbali na Kichuya, Laudit Mavugo naye alipoteza nafasi nyingi
za kufunga mbele ya JKT Ruvu ambayo wachezaji wake walicheza kwa kujihami muda
wote huku washambuliaji wake Atupele Green na Saad Kipanga wakishindwa kupiga
shuti hata moja langoni mwa Simba.
Kutoka kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, Mwadui iliibuka
na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbao FC. Bao la Mwadui liliwekwa kimiani na
Abdallah Seseme katika dakika ya 29 Kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.
Ligi hiyo inaendelea tena leo ambapo bingwa mtetezi Yanga
itashuka kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kucheza na African Lyon.
Yanga inapewa nafasi ya kuibuka na ushindi katika mechi ya
leo kutokana na ukweli kwamba bado iko vizuri kwa vile imetoka kushindana
michuano ya kimataifa.
Timu hiyo ilitupwa nje kwenye Kombe la Shirikisho na TP
Mazembe ya Congo DR baada ya kufungwa mabao 3-1 lakini hilo haliondoi ukweli
kwamba timu hiyo bado ipo vizuri na ina uwezo wa kutetea taji lake.
No comments:
Post a Comment