Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Friday, May 20, 2016

YANGA YAWASILI YAPOKEWA KISHUJAA NA MASHABIKI







JIJI la Dar es Salaam leo lilisimama kwa muda, wakati mabingwa wa Tanzania, Yanga walipowasili wakitokea Angola walikofuzu hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC).
Mamia ya mashabiki wa Yanga walianza kumiminika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam kuanzia saa tano asubuhi na hadi kufikia saa nane mchana hali uwanjani hapo ilikuwa si ya kawaida.
Pia mashabiki wa Yanga walijipanga barabarani katika maeneo mbalimbali kuanzia Uwanja wa Ndege, Kipawa, Vingunguti na Tazara, ambapo mara kadhaa msafara  wa basi la wachezaji wa Yanga uliokuwa ukiongozwa na bodaboda kadhaa ulilazimika kusimama mara kwa mara sababu ya mashabiki walikuwa wanataka kuwaona.
Kivutio kikubwa katika mapokezi hayo alikuwa kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ aliyepangua penalti ya dakika ya 90, ambaye mashabiki walikuwa wakimgombea kutaka kumbeba.
“Ahsanteni, nimefurahishwa na mapokezi, tulienda kufanya kazi ngumu, tunawaahidi raha zaidi,” alisema Dida na kuungwa mkono na Haruna Niyonzima kiungo mahiri wa Yanga na kiungo mwingine, Thabani Kamusoko.
Shamrashamra  zilizopambwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali na vijembe,  sambamba na ngoma za singeli kwa mashabiki wa Yanga, vilitawala.
Mashabiki walionekana karibu na lango la kutokea wageni mashuhuri ‘VIP’ wakisubiri kwa hamu kuwaona wachezaji ambapo saa 8.50 ndege yao ilitua ikitokea Afrika Kusini na baada ya taratibu walitoka nje ya uwanja na shangwe za: 'Dida..Dida.. Dida’ zilisikika.
Mashabiki walikuwa wenye uso wa furaha wakizingira wachezaji waliokuwa wakielekea kwenye gari lao, na bado utitiri ulisindikiza msafara huo na kusalimiana na mashabiki, ambao walikuwa wakitembea kwa miguu na wengine kwenye magari hadi kwenye Ofisi za Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam eneo la Banda la Ngozi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutua, Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema ushindi huo wametoa zawadi kwa Watanzania wote.
Alisema wanashukuru sehemu ya mafanikio hayo yametokana na Mwenyekiti Manji ambaye  amekuwa akishirikiana nao katika kuhakikisha timu inafanya vizuri.
Naye nahodha wa Yanga, Nadir Haroub alisema mechi ilikuwa ngumu kwani hata waamuzi walionekana kuibeba timu pinzani, lakini wao walijua kilichowapeleka na kupigana kwa ajili ya kufanya vizuri.
Alisema fujo zilizotokea kule hakuwahi kuziona katika maisha yake ya soka, na kwamba kwa vile wao walikuwa wanataka ushindi walicheza mpira na kutimiza lengo walilokusudia.
Timu hiyo ilitarajiwa kuondoka jana jioni kwa ndege ya kukodi kuelekea Songea ambako Jumapili itacheza na Majimaji katika kumaliza Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga Jumatano ilifuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kutokana  na matokeo ya mchezo wa uliofanyika mjini Dundo, Angola dhidi ya Sagrada Esperanca ya huko, ambapo Yanga ilifungwa bao 1-0.
 Kutokana na matokeo hayo, Yanga imefuzu kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Katika mchezo wa Dar es Salaam lilikuwa bao zuri la Simon Msuva aliyefunga kwa kichwa kufuatia majalo ya chini chini ya Geoffrey Mwashiuya, akawaamsha vitini mashabiki wa vijana hao wa Jangwani. Bao jingine lilifungwa na chipukizi Matheo Anthony kwa mkwaju mkali.
Kwa kuingia hatua ya makundi, Yanga imeandika historia mpya katika soka nchini kwa kuwa klabu ya kwanza Tanzania kufuzu hatua hiyo katika mashindano hayo, lakini ni mara ya pili kufuzu hatua ya makundi kwa mashindano makubwa Afrika baada ya kufanya hivyo mwaka 1998 katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba ya Dar es Salaam nayo ilifuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003 kwa kuitoa Zamalek ya Misri.
Yanga iliangukia Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC),  baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ililazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa mabao 2-1 Alexandria, Misri.
Ilizitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla ya kuitoa APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
Yanga sasa inaungana na miamba mingine saba Afrika na inasubiri droo ya upangaji wa makundi wiki ijayo ili ijue itakuwa kundi gani.
Timu nyingine zilizofuzu hatua ya makundi na nchi zao katika mabano ni MO Bejaoa (Algeria), Al Ahli Tripoli (Libya), FUS Rabat (Morocco), Kawkab (Morocco), ES Sahel (Tunisia), Medeama (Ghana) na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Wachezaji hao walizungumza na Mwenyekiti Manji kwa dakika kadhaa, ambapo waandishi hawakuruhusiwa kuingia na baada ya kikao hicho Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro alisema kila mchezaji ameahidiwa gari.
“Wachezaji wamezungumza na Mwenyekiti na amewaahidi kuwapa kila mmoja gari kwa hatua hii waliyofikia. Sasa ni gari gani hiyo itakuwa siku nyingine.
“Lakini nataka kuwahakikishia kwamba mtawaona wachezaji wanabadilisha maisha yao muda si mrefu. Ila ninachotaka kuwaambia sasa ni kwamba kila mchezaji ameahidiwa kupewa gari kwa kutinga hatua hii ya makundi na amewataka wasibweteke.
“Pia amewataka wasibweteke kwa kutinga makundi, bali wapambane zaidi na hata msimu ujao wacheze makundi Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Muro.

No comments:

Post a Comment