Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Thursday, May 19, 2016

YANGA KUREJEA KESHO MCHANA NA KUINGIA KAMBINIYanga  wanatarajiwa kurejea Dar es Salaam kesho mchana wakitokea Angola, ambako jana walikata tiketi ya kuingia hatua makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika.
Yanga ilifungwa bao 1-0 na wenyeji Sagrada Esperanca katika mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania hatua hiyo Uwanja wa Esperanca mjini Dundo, Angola.
Hata hivyo Yanga wanakwenda hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla wa 2-1, baada ya awali kushinda 2-0 Dar es Salaam.
Matokeo hayo Yanga inatinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza katika historia yake na inakuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufika hatua hiyo ya michuano hivyo.
Awali ya hapo, Yanga imewahi kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998, ikafuatiwa na mahasimu, Simba  mwaka 2003.  
Katika mchezo wa jana uliochezeshwa na marefa wa Madagascar, Hamada el Moussa Nampiandraza, aliyesaidiwa na Velomanana Ferdinand Jinoro na Jean Thierry Djaonirina, hadi mapumziko wenyeji walikuwa walikuwa wanaongoza kwa bao lao hilo.
Bao hilo lilifungwa na mkongwe Arsenio Sebastiao Cabungula maarufu kama ‘Love Kabungula’ dakika ya 25, baada ya mabeki wa Yanga kufanya uzembe kidogo.
Yanga walitulia baada ya bao hilo, licha ya marefa kuonekana kabisa kupendelea wenyeji na wakafanikiwa kumaliza dakika 45 za kwanza wakiwa nyuma kwa bao hilo moja tu.
Kipindi cha pili, Yanga waliachana na mchezo wa kujihamia na kufunguka kuanza kushambulia, hali ambayo ilipunguza kasi ya wapinzani wao.
Kocha Mholanzi alimtoa kiungo, Thabani Kamusoko baada ya kuumia na kumuingiza Deus Kaseke dakika ya 69 aliyemalizia vizuri.
Mshambuliaji Donald Ngoma alipoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 72.
Beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 90 na ushei baada ya kumwangusha kwenye boksi mchezaji wa Esperanca na wenyeji wakapewa penalti, ambayo hata hivyo kipa Dida aliicheza.
Baada ya kuwasili, wachezaji wa Yanga watakwenda moja kwa moja kambini kujiandaa na mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu yaTanzania Bara dhidi ya Majimaji mjini Songea Jumamosi na fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la ASFC Jumatano ijayo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga iliangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.
Yanga ilianza vizuri tu kwa kuzitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla ya kuitoa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Vincent Bossou, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Simon Msuva/Geoffrey Mwashiuya dk90, Thabani Kamusoko/Deus Kaseke dk69, Donald Ngoma, Amissi Tambwe/Kevin Yondan dk89 na Haruna Niyonzima.