ILI mmiliki wa aweze kupata leseni lazima awe ana miliki klabu moja kwenye ligi moja, kila klabu lazima iwe na programu endelevu za vijana na uwanja wa mazoezi unaokidhi viwango.
Hayo yalibainishwa jana na Mkufunzi wa Shirikisho la Vyama vya soka barani Afrika (CAF) Amanze Uchegbulanm kwenye mafunzo ya leseni za klabu za Ligi Kuu na Ligi daraja la kwanza Tanzania Bara iliyofanyika jana Dar es Salaam.
“Agizo la CAF ni kuwa kila klabu inayoshiriki michuano ya kimataifa yaani Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho lazima iwe imepata leseni ambayo itaipa nafasi ya kushiriki michuano inayoandaliwa na CAF, na kwa klabu ambayo haitatimiza mahitaji ya kupata leseni hiyo haitaweza kushiriki michuano ya kimataifa”, alisema Uchegbulanm.
Pia Uchegbulanm alisema CAF itafuatilia kuona kweli kama klabu inayocho kiwanja kinachokidhi vigezo ikiwa ni kuwa na sehemu ya vyumba vya kubadilishia nguo na sehemu ya kupumzisha majeruhi, programu za vijana pamoja kuwa na sekratarieti na mahesabu yaliyokaguliwa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) Yahya Mohamed alilishukuru CAF kuipatia mafunzo ya leseni za klabu, kwani itasaidia kuleta ufanisi kwenye uendeshaji wa mpira wa miguu
“Uendeshaji wa mpira wa miguu duniani umebadilika, mabadiliko haya yapo katika nyanja zote za uongozi (utawala), miundombinu, kitu ambacho kwa sisi Tanania tumeshaanza kuendana na mabadiliko hayo, na sasa kupata kwetu semina hii kutawafanya viongozi wengi kufahamu umuhimu wa leseni za vilabu na kufanyia kazi mapungufu yaliyokuwepo” alisema Yahya.
Semina hiyo ya Leseni kwa Vilabu itakayofanyika kwa siku mbili inaendeshwa na wakufunzi watatu kutoka CAF ambao ni Dr. Bolaji Ojo-Oba na Amanze Uchegbulanm toka Nigeria na Othman Mohamed kutoka nchini Sudan.
No comments:
Post a Comment