Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Wednesday, May 25, 2016

YANGA YATWAA KOMBE LA SHIRIKISHO NA KUONDOKA NA KITITA CHA MILIONI 50



NI Yanga ya kimataifa na mataji. Pengine ndivyo unavyoweza kuzungumzia matokeo ya mchezo wa fainali ya Kombe la FA kati ya Yanga na Azam uliochezwa leo  Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Kulingana na kanuni za mashindano hayo, bingwa wa Kombe la FA huwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC) msimu ujao, hivyo kwa ushindi wa jana Yanga ingepata fursa ya kuwakilisha nchi katika michuano hiyo.

Hata hivyo, kwa vile Yanga tayari imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara itawakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo ni mikubwa kwa ngazi ya klabu na kanuni kuipa Azam nafasi ya kucheza Kombe la CAF CC.

Yanga ilipata bao la kwanza dakika ya tisa, mfungaji akiwa Amis Tambwe kwa kichwa akiunganisha krosi ya Juma Abdul, bao lililofuatiwa na mashambulizi makali kila upande.

Makipa Deogratius Munishi ‘Dida’ wa Yanga na Aishi Manula wa Azam, ambao pia ni makipa wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwa nyakati tofauti jana walionesha uwezo mkubwa wa kupangua michomo ya washambuliaji katika milango yao.

Dakika ya 48, Tambwe aliifungia Yanga bao la pili kutokana na pasi ya Simon Msuva kabla ya dakika moja baadaye Didier Kavumbagu aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya John Bocco kuifungia Azam bao.

Kuingia kwa bao hilo kulionekana kuwachanganya Yanga ambao katika dakika ya 81 walipata bao la tatu kupitia kwa Deus Kaseke aliyefunga bao la tatu baada ya kupokea pasi ya Msuva. Kwa ushindi huo, Yanga imetwaa kombe hilo na kitita cha Sh milioni 50.

Mara ya mwisho Kombe la FA lilifanyika mwaka 2002 na JKT Ruvu Stars ya Pwani ikaibuka bingwa baada ya kuifunga Baker Rangers ya Magomeni kwenye fainali.

Wakati huohuo, kocha wa Yanga, Hans Pluijm amesema hana hofu yoyote na timu ilizopangwa nazo Yanga katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC) hatua ya makundi.

Juzi Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilipanga ratiba ya michuano hiyo, ambapo Yanga ipo Kundi A pamoja na mabingwa wa zamani wa Afrika, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Medeama ya Ghana na MO Bejaia ya Algeria.

Akizungumza na gazeti hili,  Pluijm alisema anaijua vizuri Mazembe na Medeama, kwa sababu amewahi kukutana nazo mara kadhaa akiwa na timu tofauti, hivyo haoni kama zitamsumbua katika mipango ya kucheza nusu fainali ya michuano hiyo.

“Timu ambayo inaweza kutusumbua kwa sababu siifahamu vizuri ni Bejaia ya Algeria, lakini baada ya ratiba kutoka tumeanza mikakati ya kuimarisha kikosi changu,” alisema Pluijm.

Alisema Yanga ni moja ya timu kubwa na ndiyo maana imekuwa katika nane bora Afrika, hivyo haoni sababu ya kuwa na presha kwani wana uwezo mkubwa wa kufanya vizuri kutokana na mikakati waliyo nayo.

Katika michuano hiyo, Yanga itafungua dimba na Mouloudia Olympique Bejaia nchini Algeria Juni 17 na itacheza na TP Mazembe Dar es Salaam kati ya Juni 27 na 28 mwaka huu kabla ya kumaliza hatua ya makundi pia nyumbani Julai 15 kwa kuvaa na Medeama ya Ghana.


No comments:

Post a Comment