FIFA imezipiga marufuku Klabu za Spain Real Madrid na Atletico Madrid kusaini Wachezaji wapya kwa vipindi viwili vijavyo vya Madirisha ya Uhamisho kutokana na kukiuka Sheria za Uhamisho wa Kimataifa na Usajili wa Wachezaji wa chini ya Miaka 18.
Adhabu hii haihusiki na kipindi cha sasa cha Dirisha la Uhamisho la huu Mwezi Januari lakini baada ya Dirisha hili kufungwa Real na Atletico hawaruhusiwi tena kusajili Wachezaji wapya hadi mwishoni mwa Msimu wa 2016/17.
Pia Klabu hizo zimepigwa Faini na Atletico wanatakiwa kulipa Pauni 620,000 na Real Faini yao ni Pauni 250,000.
Adhabu za aina hiyo kutoka FIFA ziliwahi kuikumba Barcelona ambapo walifungiwa kusaini Wachezaji wapya kwa Mwaka mzima Mwezi Aprili 2014 kwa kosa hilo hilo la kukiuka Sheria za Uhamisho wa Kimataifa na Usajili wa Wachezaji wa chini ya Miaka 18.
Kufuatia Adhabu, Barcelona walikata Rufaa kwa FIFA na baadae kwa CAS [Court of Arbitration for Sport], Mahakama ya Usuluhishi Michezoni, lakini Rufaa zao zote zikatupiliwa mbali na wakatumikia Adhabu yao.
Msemaji wa FIFA amefafanua kuwa Real na Atletico zinaweza kusaini Wachezaji wapya wakati wa Adhabu zao lakini Wachezaji hao hawatasajiliwa.
Na hivyo ndivyo walivyofanya Barcelona kwani waliwanunua na kuwasaini Arda Turan kutoka Atletico na Aleix Vidal kutoka Sevilla lakini Wachezaji hao hawakusajiliwa na hivyo hawakuweza kucheza hadi hii Januari baada adhabu yao kumalizika.
No comments:
Post a Comment