YANGA imezidi kuchanja mbuga kuelekea kutetea taji lake la Ligi Kuu baada
ya jana kuifunga Mbeya City mabao 3-0.
Ushindi huo umeifanya
Yanga ifikishe pointi 33 kwenye msimamo ikiwa kileleni.
Mshindani wake katika
kuwania taji hilo ni Azam ambayo haijacheza mechi mbili ikiwa na pointi 29.
Azam leo inacheza na
Kagera Sugar, na ikishinda itaikaribia zaidi Yanga. Azam imecheza michezo
pungufu mpaka sasa.
Amisi Tambwe alikuwa
shujaa wa Yanga jana baada ya kuifungia mabao mawili huku moja likifungwa na
Thaban Kamusoko.
Tambwe alifunga bao
la kwanza katika dakika ya 36 kwa shuti kali baada ya kuunganisha pasi nzuri ya
Simon Msuva.
Tambwe tena alicheka
na nyavu kufunga bao la pili katika dakika ya 65 kwa krosi ya Haji Mwinyi.
Dakika moja baadaye
Thaban Kamusoko alifunga bao la tatu akitengenezewa na Msuva tena.
Mechi hiyo ilipooza
kipindi cha kwanza kabla ya kuchangamka katika kipindi cha pili huku Yanga
wakionekana kuutawala mchezo.
Kutoka kwenye uwanja
wa Kambarage Shinyanga Simba imeendelea kutoa sare baada ya kutoka 1-1 na
Mwadui.
Hiyo ni sare ya tatu
kwa Simba baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Azam, na 1-1 na Toto Africans.
Mwadui ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Nizar Khalfani kabla
Simba haijasawazisha kupitia kwa mchezaji wake Brian Majwega.
Kwenye uwanja wa
Nangwanda Sijaona Mtwara Ndanda ya huko nayo iliendelea kugawa pointi baada ya
kukubali kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa JKT Ruvu.
Majimaji ya Songea,
ikiwa nyumbani uwanja wa Majimaji iliangukia pua kwa kuchapwa mabao 2-0 na
Prisons huku Mtibwa Sugar ikitumia vyema uwanja wake wa Manungu kwa kuichapa
Mgambo JKT mabao 3-0.
Kwenye uwanja wa
Mkwakwani Tanga, wagosi wa Kaya Coastal Union walipigwa mabao 3-1 na Stand
United.
No comments:
Post a Comment