KLABU za Simba na Azam FC zinazoshiriki ligi kuu Tanzania bara zimemalizana kuhusu mchezaji wa Brian Majwega.
Klabu hizo miezi michache iliyopita vilikuwa kwenye vita ya kumuwania mchezaji Ramadhani Singano ‘Messi’ huku Simba ikidai mchezaji huyo bado alikuwa ana mkataba nao lakini Azam ilimnasa baada ya mkataba huo kuvunjwa na TFF na Messi kusajiliwa na Azam kama mchezaji huru.
Safari hii kibao kilihamia kwao baada ya kuingia mgogoro na mchezaji wao Brian Majwega baada ya mchezaji huyo kusugua benchi kwa muda mrefu hali iliyopelekea aamue kutimkia zake kwao Uganda na aliporejea nchini akaomba kufanya mazoezi na kikosi cha Msimbazi.
Baada ya kocha wa Simba Dylan Kerr kuvutiwa na mchezaji huyo ndipo mishemishe za kumsajili zikaanza lakini Azam waliposhtukia dili hilo wakatangaza kuwa bado wana mkataba na mchezaji huyo na kwamba alitoroka na kuacha kazi yake kwenye timu hiyo na endapo Simba wakimsajili basi wao watawachukulia hatua.
Jana viongozi wa pande zote mbili wakakutana ili kuzungumzia sakata hilo na wakafikia makubaliano kwamba mchezaji huyo apewe ruhusa ya kuvaa uzi mweupe na mwekundu na kuanza kuitumikia klabu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Msimbazi, Kariakoo, Dar es Salaam.
Ili kupata uhakika zaidi mtandao huu ukamtafuta afisa habari wa Azam FC Bw. Jafar Idd ili athibitishe taarifa za Azam kutoa baraka zake kwa mchezaji huyo kujiunga na ‘mnyama’ naye bila hiana akaweka mambo hadharani.
“Brian Majwega alikuwa na mkatba halali na klabu ya Azam lakini tunashukuru viongozi wa Simba wamekuwa waungwana na wametumia busara baada ya kujua ni kweli mchezaji huyo ana mkataba na Azam walichokifanya ni kurudi chini na kuamua kuja kwenye meza ya mazungumzo na Azam”, amesema msemaji wa Azam Jafar Idd.
“Taratibu zilianza jana kati ya viongozi wa Simba pamoja na viongozi wa Azam na kwamba hivi sasa Brian Majwega ni mchezaji halali wa Simba baada ya Simba kutumia uungwana wa kukaa chini na Azam na kuzungumza suala hili kwenye taratibu zinazokubalika za mpira tumelimaliza na tumempa ruhusa Majwega kwenda kucheza Simba”.
Majwega alisafiri na kikosi cha Simba ambacho kipo visiwani Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya ligi kuu inayotarajiwa kuendelea December 12, 2015 ambapo siku hiyo Simba itacheza dhidi ya Azam FC kwenye uwanja wa taifa.
No comments:
Post a Comment