TIMU ya African Sports ya Tanga, imewapa raha wapenzi wa
Tanga baada ya kumaliza ligi kwa kuifunga Friends Rangers ya Magomeni mabao 2-1
kwenye mchezo wa kufunga pazia wa ligi daraja la kwanza uliochezwa Uwanja wa
Karume jijini Dar es Salaam jana.
Katika mchezo huo ambao ulitawaliwa na vituko vya mashabiki
wa Friends Rangers, ulishuhudia African Sports wakijipatia bao la kwanza dakika
ya 12 na kiungo mshambuliaji, Ramadhan Msheli baada ya kuwatoka mabeki wa
Friends Rangers.
Baada ya bao hilo wachezaji wa Friends Rangers walijitahidi
kusawazisha bao lakini walijikuta wakienda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao hilo
moja
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko
ambayo yaliongeza uhai kwa Friends Rangers na kujikuta wakipata bao dakika ya
46 lililofunga na mshambuliaji Ahmad Abas kwa shuti la mbali akiwa nje ya eneo
la penati.
African Sports baada ya kuona Friends Rangers wamesawazisha
walicharuka na kuanza kuliandama lango lao na kufanikiwa kupata bao la ushindi
lililofungwa na mshambuliaji James Mendi baada ya kuunganisha krosi ya Ally
Ramadhan.
Akizungumza baada ya mchezo, kocha wa African Sports, Joseph
Lazaro, alisema anawashukuru wachezaji, benchi la ufundi pamoja na uongozi kwa
ushirikiano walionesha hadi kufanikisha timu kupanda daraja.
“Nawashukuru wachezaji kwa usikivu na ushirikiano wao tangu
tulipoanza ligi na uongozi kwani umesaidia timu kufanya vizuri na nawahakikishia mashabiki wa Tanga kuwa
tuna timu nzuri ambayo inakwenda kupambana ligi kuu na siyo kwamba tunaingia na
kutoka”, alijigamba Lazaro.
Timu ya Majimaji ya Songea imeungana na African Sports
kupanda ligi kuu kwa kundi A kwa msimu ujao huku timu ya Villa Squad ikishuka
daraja la pili baada ya kumaliza ligi ikishikilia mkia kwa kundi A ikiwa na
pointi 14.
Michezo ya kundi B inatarajiwa kumalizika wikiendi ijayo
ambapo Mwadui FC imeshapanda ikiwa na pointi 43 japo ina mchezo mmoja na kuacha
ushindani kwa timu za Toto African yenye pointi 39 na JKT Oljoro 41, kila moja
ikiwa imebakia na mchezo mmoja na kuicha Green Warriors ikihesabiwa kuwa
imeshuka daraja baada ya kuwa ina pointi 11.
African Sports |
Benchi la Friends Rangers |
No comments:
Post a Comment