Timu ya Taifa ya Tanzania ya mpira wa
ufukweni (beach soccer) imepangiwa kucheza na Kenya katika raundi ya kwanza ya
michuano ya Afrika kwa ajili ya fainali za Afrika za michuano hiyo zitakazofanyika
Aprili mwaka huu nchini Shelisheli.
Mwenyekiti wa Kamati ya Beach Soccer,
Ahmed Idd Mgoyi amesema jijini Dar es Salaam, leo kuwa Tanzania itaanzia
ugenini ambapo mechi ya kwanza itachezwa kati ya Februari 13 na 15 mwaka huu
nchini Kenya.
Mechi ya marudiano itafanyikaa nchini
kati ya Februari 20 na 22 mwaka huu. Iwapo timu ya Tanzania itasonga mbele,
katika raundi ya pili itacheza na Misri ikianzia nyumbani kati ya Machi 13 na
15 mwaka huu.
Mgoyi alisema maandalizi ya Tanzania
kushiriki kwenye mashindano hayo yameanza ambapo timu ya Tanzania Bara itacheza
na Zanzibar ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kupata kikosi kimoja kitakachoingia
kwenye michuano hiyo ya Afrika.
Alisema benchi za ufundi la timu ya
Tanzania litaongozwa na John Mwansasu wakati Msaidizi wake ni Ali Shariff
'Adolf' kutoka Zanzibar, na Meneja wa timu hiyo ni George Lucas. Wote hao
walishiriki kwenye kozi ya ukocha wa beach soccer iliyoendeshwa mwaka jana
nchini na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Kocha Mwansasu atatangaza timu ya
Tanzania Bara, Januari 19 mwaka huu, na mazoezi ya pamoja na timu ya Zanzibar yatafanyika
Januari 24 na 25 mwaka huu.
Wachezaji wa timu ya Tanzania Bara
watatokana na michuano ya beach soccer iliyofanyika mwaka jana ikishirikisha
timu za vyuo vya elimu ya juu vya Mkoa wa Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment